17 December 2010

Mwalusako: Niombeni radhi

*Atoa siku saba, vinginevyo...

Na Elizabeth Mayemba
SAKATA la ufujaji wa fedha za usajili sh.milioni 100, zilizotolewa na mdhamini Mkuu wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji, limezidi kuchukua sura mpya, baada ya Katibu Mkuu wa klabu hiyo Lawrence Mwalusako kutaka aombwe radhi ndani ya
siku saba.

Kauli kama hiyo ilikuwa ikitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party, Augustino Mrema wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani miaka ya 90.

Hivi karibuni kuna habari zilizoenea kwamba, uongozi wa Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu, Mwalusako, ulichukua sh. milioni 100, kutoka kwa Manji, kwa ajili ya usajili wa dirisha dogo, hali inayodaiwa kuwa, zimetumika vibaya, na hivyo zitolewe ufafanuzi wa matumizi yake.

Akizungumza Dar es Salaam jana,  Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwalusako alisema habari hizo zimelenga kumchafua mbele ya wana-Yanga wote, jamaa zake na familia yake, hivyo ametaka aombwe radhi ndani ya siku saba, vinginevyo ataenda mahakamani na kudai fidia ya sh.milioni 150.

"Hata siku moja siwezi kutumia fedha za klabu yangu kwa matumizi yangu binafsi, na taarifa za kusema kwamba,  nimefuja fedha hizo, zimenidhalilisha sana, nataka kuombwa radhi ndani ya siku saba, vinginevyo naenda mahakamani," alisema Mwalusako.

Akitoa ufafanuzi wa fedha hizo, Mwalusako alisema ni kweli alipokea hundi ya sh.milioni 100, kutoka kwa mdhamini wao kwa ajili ya usajili, ambapo mahesabu yao yalikuwa ni kusajili wachezaji watatu.Alisema katika fedha hizo, sh.milioni 25 walitumia kusajili wachezaji wao wawili, Mzambia Davies Mwape na Juma Seif  'Kijiko' wa JKT Ruvu.

Mwalusako alizidi kufafanua kwamba,  kuna hundi ya sh.milioni 40 ambayo aliionesha kwa waandishi wa habari kwamba, haijatumika na sh.milioni 35 zipo katika akaunti ya klabu yao.

Alisema huo ndio ufafanuzi wa kiasi hicho cha fedha na kuwataka wanachama wote ambao nao walitaka kujua matumizi hayo, kujua ufafanuzi huo alioutoa ili kuondoa msemo wa kwamba, fedha hizo amezitafuna.

1 comment:

  1. kaka Laurence mbona husemi nani utampeleka mahakamani? usije ukawa unaogopa kivuli chako. Chapa kazi, tunza fedha za kilabu, tupo nyuma yako. Nakujua wewe ni msitarabu.

    ReplyDelete