27 December 2010

Kijiji chadai hakina maji tangu uhuru

Na Raphael Okello, Rorya

WAKAZI wa Kijiji cha Panyakoo, Kata ya Goribe wilayani Rorya mkoani Mara wameilalamikia serikali kwa kushindwa kuwapatia huduma ya maji ya mifugo na matumizi ya majumbani tangu uhuru na kusababisha kufuata huduma hizo katika nchi jirani ya
Kenya.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki baadhi ya wakazi hao wamesema kutokana na ukosefu wa maji kijijini hapo na vijiji jirani vya Ng’ope, Charya na Nyamusi, wananchi wanalazimika kunywesha mifugo yao katika malambo ya Olasi nchini Kenya ambapo licha ya kutozwa fedha katika huduma hizo, lakini pia wanateseka kutembea umbali mrefu wa wastani wa km 30 kwenda na kurudi pamoja na mifugo yao.

Wamedai kutokana na hali hiyo baadhi ya mifugo yao imekuwa ikipotea au kuibwa na watu wasiojulikana hivyo wameiomba serikali kuwachimbia lambo kwa ajili ya mifugo yao na visima kwa matumizi ya nyumbani.

Wananchi hao wamekuwa wakipata maji katika msimu wa mvua katika visima vifupi vya asili kwa matumizi ya nyumbani, na Mto Ondoche kwa mifugo, lakini vyanzo hivyo huchukua muda mfupi tu kukauka mara baada ya msimu wa mvua kumalizika.


“Kutokana na ukame huu tunategemea kunywesha mifugo yetu katika malambo ya Kenya kwa sababu tayari mto Ondoche umekauka ,kwa hiyo tuna shida kubwa sana,” alisema Bw. Adundo Oleng’a ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Habari kutokana kijijini hapo zinaeleza kuwa katika juhudi za kuondokana na adha hiyo, miaka mitatu iliyopita, uongozi wa serikali Kijijini hapo uliwachangisha fedha wananchi kwa ajili ya kuchimba lambo lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na hawajui fedha hizo zimefanya kazi gani.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Panyakoo, Bw. Elias Bunde hakupatikana kutoa ufafanuzi zaidi juu ya matumizi ya fedha hizo zinazodaiwa kuchangishwa kwa lengo la kumpa kiongozi mmoja aliyeahidi kuleta mitambo ya kuchimba lambo kijijini hapo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia akina mama na wasichana wakitembea umbali mrefu kutafuta maji ambapo walieleza kuwa wamekuwa wakifanya hivyo hadi saa 3:00 usiku.

Walimtaka mbunge wa jimbo hilo, Bw. Lameck Airo kuhakikisha kuwa anawapatia maji ili waondokane na adha hiyo.

Kijiji hivyo ni moja ya vijiji vilivyoanzishwa mwaka 1974 ambapo tangu hapo hadi leo hakuna kisima cha maji wala lambo kwa ajili ya matumizi ya watu na mifugo yao.

1 comment:

  1. sio ninyi pekee yenu, nchi imevamiwa na waporaji wa mali zetu za asili. kila mwaka wanakopa fedha kutoka kwa wafadhili wanadhalilisha nchi, pesa wanazitumia wao na familia zao. nchi inabaki na madeni, badala ya kuzitumia kwa masuala hayo ya maendeleo, mura lete lile lijeshi tuwaonyeshe kazi

    ReplyDelete