03 December 2010

Kanisa lachomwa moto Ngara

Na Theonestina Juma, Ngara

KANISA la Pentekoste ambalo waumini wake walikimbia nyumba zao na kuishi porini baada ya kukataa kunyunyiziwa dawa ya kuua mbu limechomwa moto na mwananchi mmoja mwenye hasira kwa madai kuwa serikali imeshindwa kumchukulia hatua mchangaji wa
kanisa hilo.

Waumini wa kanisa hilo, walikimbia nyumba zao na kupiga kambi katika pori la Nyakafandi, Kata ya Mugaza wilayani hapa kwa madai kuwa kukubali nyumba zao kunyunyiziwa dawa hiyo ni kinyume, kwa kuwa mlinzi wao ni Mungu pekee.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia waumini hao wakiwa na watoto wao katika pori hilo.Mchungaji Annamaria Mulengera, alisema Kanisa lao ambalo lilijengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi lilichomwa moto Novemba 7, mwaka huu saa 1:00 jioni.

Alimtaja mwanamume aliyechoma kanisa lao, ambaye mke wake ni miongoni mwa waumini wa kanisa hilo kwa madai kuwa mchungaji amevunja ndoa yake.Alisema mwanamume huyo alikuwa akiwatembelea mara kwa mara lakini baadaye wamebaini kuwa alikuwa akiwachunguza jinsi wanavyoishi ili kutimiza lengo lake la kuchoima kanisa.

Hata hivyo, mchungaji huyo alisema hawakuripoti tukio hilo popote kwa kuwa wanamwamini Mungu kwa kila jambo na kwamba aliyefanya tukio hilo anatumiwa na shetani.Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bulinda Kijiji cha Mukubu, Bw. Thobias Nkenke, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kukiri kuwa mwanamume aliyetajwa ndiye aliyefanya kitendo hicho.

Alisema kuwa mwanamume huyo alifikia maamuzi hayo ya kuchoma moto kanisa hilo baada ya mkewe kumkimbia na kuhamia katika pori hilo pamoja na mwanawe mwenye umri wa miaka mitano.

Alisema mtuhumiwa huyo alidai kuwa mkewe alikataa kurejea nyumbani na mwanaye kwa madai kuwa wametokewa na sauti ya Mungu kuwa anakaribia kushuka.Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Bw. Salum Nyakoji alikana kuwa na taarifa za kanisa hilo kuchomwa moto.Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kagera, Vitus Mlolere, aliahidi kufuatilia kwa karibu suala hilo.

3 comments:

  1. Mh! kuna kazi sana juu ya Imani ya Binadamu kwa Mungu wake! wengine walihamia Dar aiport kusubiri kwenda nje kuhubiri na ppt zao ni biblia! Eh Mungu we! tusaidie!

    ReplyDelete
  2. safi Kabisa, Msipoangalia Vizuri akina kibwetele ni wengi

    Mking'amua mapema ni kuchoma tuuuuuuuuuu

    ReplyDelete
  3. serikali inangoja nini kumchukulia hatua huyo mchungaji? hata kama katiba ya nchi inatoa uhuru wa kuabudu lakini sasa hii kali. mwishowe atatokea mtu mwingine na panga kumkatakata huyo mchungaji kwa madai ya kuishi na mkewe huku yeye akiwa na shida naye

    ReplyDelete