03 December 2010

Nyalandu: Kuchapa kazi kutajengea nchi heshima

Na Tumaini Makene

WATANZANIA wametakiwa kuamsha ari ya kufanya kazi kwa bidii, na kuondoa hofu, huku wakishirikiana na wawekezaji wengine kutoka nje kutumia fursa zilizopo kujiendeleza na kuiendeleza nchi ili kujenga upya taswira ya Tanzania kiuchumi.Wameambiwa kuwa
nchi inazo fursa nyingi za wenyeji na wageni kuwekeza katika nyanja mbalimbali, huku pia serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ikihakikisha kuwa fursa zinazopatikana nje ya nchi kutokana na uhusiano wa nchi marafiki, zinatumika ipasavyo.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Bw. Lazaro Nyalanda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya mkutano mfupi na mwenzake katika nafasi hiyo, kutoka Viet Nam, Bw. Le Duong Quang.

Bw. Quang yuko nchini akiongoza ujumbe wa kiserikali na wafanyabiashara wakubwa kutoka Viet Nam, kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi hiyo, kiuchumi, kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizo mbili.

"Watanzania waache kulalamika tu...tena wajue kuwa wakati wa watu kulala mpaka saa 2 au mpaka saa 4 umeshapita, huu ni wakati wa kufanya kazi...mtu aamuke mapema alfajiri, apange mambo yake ya kufanya siku hiyo. Unajua ukikuta mtu analalamika lalamika sana, huko nyumbani, katika ofisi za serikali, katika taasisi, maana yake rahisi ni kuwa hana kazi za kufanya.

"Tufanye kazi, tushirikiane na watu, wageni kama hawa, tunazo fursa nyingi tu nchini na nje ya nchi...tujenge spirit (ari) ya kufanya kazi...hiyo ndiyo ita-rebrand (kujenga upya taswira) Tanzania, tusonge mbele. Hakuna aliyeamini kuwa iko siku tunaweza kuuza bidhaa za fedha nyingi Kenya, kuliko wao walivyouza kwetu," alisema Bw. Nyalandu.

Akizungumza na Bw. Quang mapema, na hata wakati wa kuzindua mazungumzo baina ya jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Viet Nam, Bw. Nyalandu alisema kuwa Tanzania inazo fursa nyingi katika uwekezaji na hivyo inafurahi nchi marafiki wanapojitokeza kushirikiana kimaendeleo, kwa faida ya pande mbili.

Alisema kuwa mwekezaji anapowekeza nchini ana uhakika wa soko kubwa, hivyo akawakaribisha kuwekeza na kufanya biashara na Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, madini, viwanda, hususan vile vya usindikaji ili kuongeza thamani ya bidhaa katika soko la dunia.

Kwa upande wake, Bw. Quang alisema kuwa nchi yake inafurahia uhusiano wa muda mrefu na Tanzania kiuchumi, ambapo wafanyabiashara aliombatana nao wakiwakilisha makampuni makubwa huko kwao, wangependa kuwekeza katika sekta ya uchimbaji madini na zana za kilimo.

"Pia ni wakati mwafaka sasa Tanzania kuwa na ofisi ya ubalozi nchini Viet Nam, ili kuondoa usumbufu wa kupata visa na masuala mengine...uchimbaji wa madini na utengezaji wa zana za kilimo ni masuala ambayo nchi hiyo ingependa kuwekeza kwa kiasi kikubwa," alisema Bw. Quang.

Wakati huo huo, John Daniel anaripoti kuwa Bw. Nyalandu amesema siku za wamachinga wa kichina wanaofanya shughuli zinazotakiwa kufanywa na wazalendo zinahesabika.Akijibu maswali ya waandishi wa habari Ofisini kwake jana, Bw. Nyalandu alisema katika kipindi hiki wizara hiyo itaangalia na kufuatilia kwa umakini sheria za biashara ili kuondoa kero hiyo.

"Napenda niwahakikishie kuwa ipo sheria inayozungumzia kazi zipi zifanywe na wageni wa nje na zipi zifanywe na Watanzania pekee."Kama kuna wamachinga wa Kichina pale Kariakoo na wanafanya kazi ambazo hawaruhusiwi kisheria basi muda wao ni mfupi sana," alisema Bw. Nyalandu.

Hata hivyo aliwataka Watanzania kubadilika na kuacha tabia ya kulalamika bila kufanya kazi na kwamba muda wa kulala hadi saa mbili au saa nne kisha kulalamikia maisha magumu ni mwisho.

No comments:

Post a Comment