03 December 2010

Mali zilizookolewa na polisi Mbeya 'zayeyuka'

Na Rashid Mkwinda, Mbeya

WAFANYABIASHARA wa Soko la Uhindini lililoungua moto usiku wa kuamkia jana jijini Mbeya wamelilaumu Jeshi la Polisi kuwa baadhi ya askari wa jeshi hilo wamehusika kupora mali zilizokuwa zinaokolewa wakati linateketea. Mwenyekiti wa Soko hilo, Bw. Emili Mwaituka alisema
kuwa kuna uwezekano mkubwa wa askari polisi kuhusika na uporaji wa mali za wafanyabiashara hao kwa kuwa idadi ya safari za kubeba mali hizo kutoka sokoni haziwiani na mali zilizokuwepo kituo cha polisi.

Bw. Mwaituka alisema kuwa usiku wa kuamkia juzi askari polisi walitumia magari yao kuokoa mali zilikokuwa hatarini kuteketea kwa moto, lakini walipofika katika kituo cha polisi mali walizozikuta hazilingani na zilizookolewa na askari hao.

"Askari tuliwaona ni wasaidizi wetu katika kuokoa mali zetu, tulitarajia kukuta mali zote zilizoporwa kituo cha polisi. Tulichokikuta ni vitenge vichache na khanga," alisema Bw. Mwaituka.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile alisema kuwa iwapo zipo tuhuma hizo za uporaji, mtu yoyote mwenye ushahidi  autoe ili hatua za kisheria zifuatwe.Jana asubuhi Bw. Mwakipesile alikaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutathmini tatizo hilo na kuagiza wafanyabiashara wote waliokuwa wakitumia soko hilo kwa kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Mbeya kuangalia uwezekano wa kutafuta eneo mbadala kwa ajili ya kujiegesha.

Bw. Mwakipesile alisema kuwa kuungua kwa soko hilo kunatoa mwanya kwa halmashauri ya jiji kujipanga vyema kwa ujenzi wa soko jipya la kisasa, ambalo litakuwa na miundombinu ya kisasa linaloweza kukidhi matukio tofauti ikiwemo kudhibiti majanga ya moto.

Alitolea mfano kuungua kwa soko hilo kuwa ililazimika kuita tingatinga kwa ajili ya kutengeneza njia, ili magari ya zima moto yamudu kufanya kazi hiyo kwa kuwa soko hilo lilikuwa halifikiki.

Bw. Mwakipesile alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa kasoro kadhaa za utendaji wakati wa uzimaji wa moto huo, lakini jitihada zilifanyika ili kuhakikisha moto unazimwa kwa kutumia magari mawili ya zimamoto.

Moto huo ulioanza majira ya saa 2:30 usiku baada ya kuzimika ghafla kwa umeme hali ambayo inadaiwa kuwa inaweza kuwa ni chanzo cha moto huo, ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa inawezekana chanzo cha moto huo ni akina mama lishe waliouacha moto katika vibanda vyao usiku huo.

Mara baada ya moto huo kuanza magari mawili ya Kikosi cha Zimamoto yalifika eneo la tukio ambapo gari la kwanza lenye namba za usajili SM 4524 lilifika eneo la tukio likiwa na maji kidogo na gari lenye namba za usajili SM 6043 lilikuwa limekosa nafasi ya kuingia katika eneo soko hadi lilipokuja tingatinga kubomoa baadhi ya vibanda.

Soko hilo lilikuwa likitoa huduma kwa wakazi wa katikati ya Jiji la Mbeya kwa bidhaa mbalimbali ambapo wafanyabiashara wanaokadiriwa 100 vibanda vyao vimeteketea kwa moto.Kuungua kwa soko hilo kumewakumbusha wakazi wa Mbeya mwezi Desemba 2006 Soko la Mwanjelwa lililopoungua moto katika mazingira yanayofanana.

2 comments:

  1. POLE SANA AFANDE MWEMA. NAAMINI UJUMBE HUU UMEKUFIKIA.

    ReplyDelete
  2. PATRICK NGALA-OLEMONG'IDecember 3, 2010 at 11:31 AM

    Hili ni swala nyeti serikali wasije wakapuuzia,uchunguzi ufanywe haraka kujua hiyo hujuma imetokeya aje wakati vyombo vya dola ndio waliokuwa wanaokoa bidhaa wakati soko lina ungua.
    Pia halmashauri zetu za miji na jiji zijitahidi kujenga miundo mbinu rafiki wakati majanga kama haya yanatokea. hii ni pamoja na kuangalia idadi ya watu hasa kwenye masoko yetu ambayo mengine yamejengwa miaka na 1970 na 1980.
    Poleni sana wakazi wa mbeya lakini shikieni bango uchunguzi wa mali zenu zilizo potea siku hiyo hasa zile zilizo okolewa.

    ReplyDelete