06 December 2010

11 wauawa na majambazi tangu Julai

Na Prosper Kwigize, Kigoma

JUMLA ya watu 11 wamepoteza maisha katika matukio 21 tofauti ya ujambazi wa kutumia silaha za kivita wilayani Kibondo mkoani Kigoma yanayotajwa kutokea katika kipindi cha mwezi July hadi Novemba mwaka huu. Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa
Wilaya ya Kibondo, Bw. Dan Makanga wakati wa kikao cha ujirani mwema kati ya uongozi wa Mkoa wa Kigoma na wakuu wa mikoa ya Chankuzo na Ruyigi .chini Burundi, kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Kibondo.

Kikao hicho kilifanyika katika Kijiji cha Mkarazi, Tarafa ya Mabamba wilayani Kibondo, eneo la mpakani mwa Tanzania na Burundi, kikiwa na lengo la kupitia kwa kina utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyofanyika nchini Burundi mapema mwaka huu.

Awali Bw. Makanga alisema matukio ya ujambazi yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika Wilaya ya Kibondo hasa katika vijiji vya mipakani na barabara kuu ya Kasulu-Kibondo na kibondo “Nyakanazi, na kwamba wananachi wakekuwa wakipoteza mali na wakati mwigize kujeruhiwa ama kuuawa, hali inayochangia kuzorota kwa uchumi wa wilaya hiyo na mkoa wa Kigoma.

Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa katika matukio hayo majambazi yanatumia silaha kali za kivita kama SAR, SMG, LMG na mabomu ya kutupa kwa mkono ambayo yanasadikiwa
kuvushwa kutoka Burundi na kuingizwa Tanzania ambapo huuzwa au hufayiwa kazi na kisha kurejeshwa nchini Burundi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Chankuzo, Bw. Niragira Jean Berkmas na Nshimirimana Syriake wa Mkoa wa Ruyigi wamekiri kuwepo kwa mahusiano makubwa ya uhalifu unaofanyika Tanzania na raia wa Burundi, ambao hadi sasa wanatajwa kujihusisha na ujambazi.

Wakuu hao wameiomba Serikali ya Tanzania kutoa ushirikiano kwao ili kukomesha uhalifu wa kutumia silaha katika maeneo ya mipaka na kukiri kuwa watu wengi nchini Burundi wanamiliki silaha walizopora wakati wa vita na tangu kipindi hicho hawajazisalimisha.

Mkoa wa Kigoma umekuwa na desturi ya kufanya vikao vya ujirani mwema na nchi ya Burundi kwa ajili ya kujadili na kupanga mikakati ya kiulinzi katika mpaka wa nchi hizo na kubadilishana taarifa za uhalifu.

2 comments:

  1. Waziri Nahoda hio kazi changamkia. Mrema ni waziri pekee aliekuwa na legacy ya kuimudu wizara hii. Majambazi, rushwa ktk sehemu nyeti za serikali ni mambo yanaotia doa Tz.

    Lazima uzifanyie mabadiliko idara zote za wizara kwani watendaji waandamizi wanashindwa kuboresha utendaji wa majukumu ya wizara.

    Kwa kuanzia:-
    -lazima uboreshe kikosi cha kuzuia rushwa
    -Anzisha kitengo cha kufyeka uhalifu na ujambazi
    -Watake wakuu waandamizi kutengeneza strategy ya kufanikisha utendaji ktk idara zao
    -Wape muda wa utekelezaji
    -Fuatilia utekelezaji wao
    -Weka website au forum ya kuwataja mafisadi ukiwa na lengo la kuleta transparency ktk kazi
    -Wapatie watendaji vitenda kazi, nk.

    wachangiaji wanaweza kupanua orodha ya mambo muhimu ya kufatialia. Na utapofanya hivo, hadhi yua wizara na taifa itarejea katika kipindi kifupi...

    ReplyDelete
  2. Waziri Nahodha ujambazi wa kuteka magari katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Mwanza na Shinyanga inayopakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi imekuwa ni kidonda ndugu.

    Jitihada za makusudi zinatakiwa kufanywa kuondoa hali hii. Sehemu hii ya nchi imekuwa si salama labda kama ilivyo Somalia. Majambazi yamefanya maeneo haya kuwa yao na kufanya wanavyotaka kila wanapoamua.

    Waziri Nahodha hebu rejesha heshima ya nchi yetu kwa kuweka mikakati ya kudumu ya kuwaondolea mbali na kuwatokomeza majambazi hawa wasiokuwa na chembe ya utu hata kidogo.

    Mabingwa kama kina kamanda Tossi wasielekezwe kwenye maeneo haya katika operation zima moto baada ya matukio peke yake kama ambavyo imekuwa siku zote. Kuwe na mabingwa kama hawa wa kudumu katika maeneo haya kama ilivyo kwa kanda maalumu Dar es Salaam. Kuwe na kikosi cha kanda maalumu kwenye hii misitu chenye kujitegemea. Kipatiwe vitendea kazi kama helkopta na kikosi kamili mfano cha mbwa kufuatilia nyendo za majambazi hawa misituni. Washirikishwe pia askari wa Jeshi la wananchi (JWTZ) na usalama wa taifa.

    Hebu wakati wa kumaliza tatizo hili uwe ni sasa.

    ReplyDelete