26 November 2010

Wasomi waibua mawazo ya Nyerere kuchochea maendeleo.

Na Mwandishi wetu, Morogoro.

VIJANA wa Kitanzania wametakiwa kujifunza na kuelewa mafundisho na mawazo ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere kwa manufaa ya taifa.Hayo yalisemwa na
Prof. Joseph Kuzilwa, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alipokuwa akizungumza katika siku maalumu ya chuo hicho ya kuadhimisha kumbukumbu ya Mwl. Nyerere (Nyerere Day) jana mjini Morogoro.

“Mwalimu Nyerere alikuwa mwalimu na mtu wa kuigwa sio tu Tanzania bali Afrika na dunia nzima,” alisema na kuongeza kuwa mchango wake katika ukombozi nchi za Afrika na kupigania maendeleo unafahamika.

Aliongeza kuwa wengi wa vijana wa sasa walikuwa hawajazaliwa kipindi cha Mwalimu Nyerere na hivyo siku hii ya Nyerere chuoni hapa inatoa mwanya kwa vijana hao kujua historia kupitia majadiliano, na kusoma maandiko mbalimbali ya kiongozi huyo kwa maendeleo ya taifa.

“Ni kweli hatunaye tena lakini mawazo yake yapo, hayajafa. Vijana lazima wajifunze,” alisema.

Ikiwa imetayarishwa na Tasisi ya Maendeleo ya chuoni hapo, tukio hili lilitoa nafasi kwa wanafunzi, wanazuoni mbalimbali na wafanyakazi wengine kujadili mawazo ya Mwalimu Nyerere kuhusiana na chaguzi za kidemokrasia na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu Uchaguzi wa Kidemokrasia.”

Akichangia mada, Prof. Faustin Kamuzora, Naibu Makamu Mkuu wa chuo, Utawala na Fedha, alisema kuna umuhimu kwa serikali za Afrika kutumia mfumo wa serikali za umoja wa kitaifa ili kuepuka migogoro.

“Hii itasaidie kuepuka migogoro kama ilivyoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali Afrika,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Daniel Mkude alisisitiza umuhimu wa kuenzi mawazo ya hayati Nyerere maana hayajafa na ni muhimu kwa umoja, usawa na maendeleo kwa taifa.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Peter Kopoka alisema kuna umuhimu wa kuwa na tume huru za uchaguzi ili kufikia demokrasia ya kweli kwa manufaa ya vyama vyote vya siasa.

Mzumbe imekuwa ikiadhimisha siku hii maalumu tangu mwaka 2004 kama sehemu ya kutambua na kuenzi michango mbalimbali ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa akitoa kwa nchi na mataifa mengine duniani katika uhai wake.

2 comments:

  1. Jamani kweli hawa watu wengine wanajua wanalolisema kweli ama `watu waseme nami niseme`? enzi za Nyerere tulikuwa tunapanga foleni kwa kununua chakula,kulikuwa na magendo ya chakula ,je huu ndio mfano wa uchumi tunaoutaka katika nchi hii ? Nyerere alikiri kuwa kiuchumi alifeli je kuna faida gani ya kukumbusha au kusema enzi zake kulikuwa na neema? Tuacheni hizo

    ReplyDelete
  2. Mdau hapo juu naomba kutofautiana na wewe kwa kiwango kikubwa kwa maelezo yafuatayo.
    Bahati mbaya sikubahatika kuishi wakati wa Nyerere kwani nimezaliwa miaka ya sabini mwishoni, lakini kwa kuwa mimi napenda sana kusoma hasa sera za kijamaa (Socialism/communism, kutemeana na mrengo wango) Mawazo ya Nyerere yalikua mazuri sana, shida ni kwamba popote penye ujamaa mabepari hutia udhia. Na ndicho kinachoonekana Cuba, Karea ya Kaskazini, ukiacha uchina amabko walikua wajanja kurekebisha sera na kuwa na ubepari unaomilikiwa na serikali na sio watu kama ilivyo kwa nchi za magharibi.

    Na kibaya zaidi kwamba watu mnatufanya tuone kipindi cha Nyerere kilikua kibaya, lakini hamtuambii kwamba mlikua mnasoma bure, hospitali bure kwa maeneo zilipokuwepo, kiwango cha ufisadi kilikua chini. Hayo yote hamyasemi,kwakua mnataka kuhalaisha dhamira za kujimilikisha nchi, na kuongeza kukua kwa matabaka ya udin, ukabila, kipato,n.k. Naomba tumetendee haki mwalimu kwa kuyakumbatia yale aliyoamini na tuone kwamba kufeli kwa sera zake ni matokeo ya mifumo ya kiuchumi ya dunia na si sera mbaya za mwali. We should not interpet Nyerere’s policies out of context. Kwa kuanzia naomba usome hiki kitabu Ujamaa Essays on Socialism. Julius Kambarage Nyerere.
    HAYA NDIYO YALIKUA MALENGO YA MWALIMU KATIKA KUANZISHA SERA YA UJAMAA.
    To build a society in which all members have equal rights and equal opportunities; in which all can live at peace with their neighbors without suffering or imposing injustice, being exploited, or exploiting; and in which all have a gradually increasing basic level of material welfare before any individual lives in luxury. (Nyerere, 1968, page 110)
    Asante.
    Ukitaka mjadala zaidi naweza kukupa contact zangu.

    ReplyDelete