26 November 2010

Wanne kizimbani kwa tuhuma za ujambazi.

Na Rehema Maigala.

WAKAZI wanne wa Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi ya Kinondoni kwa tuhuma za wizi wa kutumia silaha katika kesi tofauti.Mashtakiwa hao ni
Bw. Masunga Makenza (34), Bw. Yusuphy Omari (39), Bw. Juma Omari (28) na Bw. Thabit Hamisi (34) ambao wanashitakiwa mbele ya mahakimu watatu kwa nyakati tofauti, Bi. Sundi Fimbo, Bi. Jackline Rugemalira na Bi. Linna Msanga.

Waendesha Mashtaka katika kesi hizo ni Bw. Iddi Kiyogoma, Bw. Wilson Maira na Bw. Benedict Nyagabona waliadai kuwa walifanya makosa kwa siku tofauti katika maeneo ya Bunju, Mikocheni na Kariakoo.

Katika kesi ya kwanza iliyosomwa kwa Hakimu Fimbo na Mwendesha Mashtaka Kiyogoma ilidaiwa Agosti 15, mwaka huu saa tano usiku maeneo ya Bunju washtakiwa kwa pamoja waliiba vitu mbalimbali vya ofisi vyenye thamani ya sh. 21, 520,000 mali ya Zang Hong.

Katika kesi ya pili, Mwendesha Mashtaka, Willson Maira alidai kwamba washitakiwa kwa pamoja Novemba 21 mwaka huu maeneo ya Mikocheni waliiba vitu vyenye thamani ya sh. milioni 60 mali ya Chen Hua.

Kesi ya tatu iliyosomwa na Mwendesha Mashitaka Nyagabona mbele ya Hakimu Linna Msanga ilidaiwa kuwa Agosti 22 mwaka huu eneo la Kariakoo washitakiwa walimwibia Zhang Wanyong vitu vyenye thamani ya sh. milioni 50 kwa kutumia silaha na kuwatishia kuwaua ili kufanikisha wizi huo.

Washtakiwa walikana kutenda mashtaka yote yanayowakabili na walirudishwa rumande kwa kukosa dhamana hadi Desemba 6 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment