29 November 2010

Wadau wataka utungaji vitabu upitiwe upya.

 Na Grace Michael

WADAU wa elimu wameshauri kurejewa kwa  utaratibu wa utungaji vitabu vya kujifunzia na kufundishia unaoshirikisha jopo lenye watalaamu mbalimbali ili kuhakikisha vitabu hivyo vinazingatia
taaluma na kuwajenga wanafunzi.

Mbali na hayo pia wameiomba jamii kuhakikisha inakuwa na mwamko wa elimu kwa kushirikiana na walimu hasa katika kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi shuleni hatua itakayosaidia kubaini matatizo ya mwanafunzi au ya mwalimu haraka.
Hayo yalijitokeza mwishoni mwa wiki wakati wakitoa mapendekezo ya namna ya kufanya ili hatimaye elimu iweze kurejea misingi ya awali na kuondokana na ubabaishaji uliopo sasa ambapo waandishi wa vitabu wamejikita katika biashara zaidi kuliko kuzingatia taaluma.

Warsha hiyo iliandaliwa na Mtandao wa Elimu (TEN/MET) kwa kushirikiana na OXFARM ambao ulikutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakaguzi, maofisa elimu, walimu pamoja na taasisi zinazoshughulikia masuala ya elimu kwa ajili ya kujadili upatikanaji wa elimu inayomlenga zaidi mwanafunzi.

"Kama utungaji wa vitabu utarejea kama ilivyokuwa awali kwa kukutanisha wataalamu mbalimbali, mambo yasiyo na msingi au ambayo yako kinyume na taaluma hayatapita, lakini kama hali hii itaachwa elimu yetu itazidi kushuka hivyo kuna haja ya serikali kuliangalia hili kwa umakini," walisema wadau hao.

Mshiriki mwingine, Bi. Honoratha Mushi alisema kuwa wazazi wanatakiwa kuepuka tabia ya kukimbilia kununua mitihani au kufurahia matokeo anayoyapata mwanafunzi bila ya kufuatilia uwezo wa kielimu alionao mtoto.

"Tatizo kubwa lililopo sasa ni wazazi kutaka watoto wafaulu bila kuzingatia kama elimu anayoipata inampa ujuzi  wa kufikiri, kuchambua mambo, ubunifu na mambo mengine; na ndio maana hata imefikia hatua ya wazazi kushiriki katika kununua mitahani kwa ajili ya watoto.

“Hali hii itazidi kuua elimu kwa kuwa watoto watabaki wakisomea mitihani badala ya kuangalia uthamani wa elimu hiyo," alisema Bi. Mushi.

Alisema kuwa ni vyema sasa jamii ikaachana na utamaduni wa kurahisisha mambo na badala yake ishirikiane bega kwa bega katika kuhakikisha wanafunzi wanapoata elimu ambayo itawawezesha kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo hapo baadaye.

Jambo jingine lililopendekezwa ni kuhakikisha serikali inasimamia vyema namna ya kuandaliwa kwa walimu ili kupata watu wa kutoa elimu bora.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu (Ualimu), Bi. Helen Lihawa alisema umefika wakati wa kuhakikisha njia shirikishi ya kufundishia inatumika ipasavyo ili kuwafanya wanafunzi wawe na uwezo wa kuibua hoja badala ya kubaki darasani wakisikiliza.

No comments:

Post a Comment