29 November 2010

Ferguson amwagia sifa Berbatov.

LONDON, England.

KOCHA Sir Alex Ferguson amemwagia sifa mchezaji wake, Dimitar Berbatov kwa mabao yake matano aliyoifungia timu hiyo na kuifanya iondoke na ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya  Blackburn, katika mechi ya
Ligi Kuu ya England.

Mchezaji huyo raia wa Bulgaria, tangu ajiunge na Manchester United amekuwa hayupo kwenye kiwango kizuri baada ya kucheza mechi 10, bila kufunga goli walau hata moja.

Hata hivyo juzi Berbatov, amekuwa kati ya wachezaji wanne ambao wamewahi kufunga mabao matano katika mechi moja kwenye historia ya Ligi Kuu, rekodi ambayo imeifanya Manchester United kukwea kileleni mwa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu.

Berbatov, katika mchezo huo alionekana kutoa mchango mkubwa baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita, kutokuwemo kwenye kikosi kilichoumana na Wigan.

"Ni mafanikio ya ajabu," alisema Ferguson.

"Angeweza kufunga mabao sita, lakini Paul Robinson alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira dakika za mwisho," aliongeza Ferguson na akasema kuwa washambuliaji wanapokuwa hawajafunga mabao huwa hawadhani kama wanafanya kazi nzuri na mara zote, hilo ndilo linakuwa tatizo kwao lakini akasema mchezaji huyo juzi alirejea kwenye kiwango chake.

Katika rekodi hiyo, Berbatov na washambuliaji wenzake wa zamani wa Manchester United, Andy Cole, Alan Shearer na Jermain Defoe ndiyo wachezaji pekee ambao wamewahi kufunga mabao matano katika mechi moja, tangu mfumo mpya wa ligi uanzishwe mwaka 1992.

"Siwezi kuamini kama nimefunga mabao matano katika mechi moja, lakini limetokea," alisema Berbatov na kuongeza kuwa amewahi kufunga mabao mengi siku za nyuma, lakini ni muda mrefu wakati akiwa nyumbani kwao Bulgaria.

No comments:

Post a Comment