29 November 2010

Serikali kuendeleza Kili Marathon.

Na Flora Temba, Moshi.

SERIKALI ya Mkoa Kilimanjaro, imeahidi kutoa ushirikiano wake katika kuendeleza mbio za Kilimanjaro Marathon kutokana na umuhimu wake wa kukuza uchumi wa Mkoa huo.
Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Meja Jenerali mstaafu, Said Kalembo wakati wa uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon 2011, uliofanyika mjini Moshi, mwishoni mwa wiki.

“Mkoa wa Kilimanjaro kama mwenyeji wa mashindano haya ya kimataifa na ambayo yamekuwa maarufu ulimwenguni kote, umekuwa ukipokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, jambo ambalo linauingizia mkoa huu mapato mengi, hivyo kuinua uchumi wa mkoa na watu wake,” alisema.

Kalembo alisema mbali na kushiriki mbio hizo, washiriki na mashabiki wake huwa wanapata fursa za kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama hapa nchini na pia kuuona mlima mrefu kuliko yote Afrika, Kilimanjaro.

“Sisi uongozi wa Mkoa tunaahidi kushirikiana na wadhamini wa mbio hizi, Kilimanjaro Premium Lager na waratibu Executive Solutions pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha zinakuwa za kudumu,” alisema.

Aidha alitoa wito kwa uongozi wa riadha mkoani Kilimanjaro kuhakikisha inawatayarisha wanariadha wa mkoa huo, ili waweze kuuwakilisha vyema na kushinda medali nyingi iwezekanavyo.

Mkuu huyo wa Mkoa, pia aliwapongeza wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Kilimanjaro Premium Lager pamoja na wadhamini washiriki, ambao ni Vodacom, Tanga Cement, DT Dobie, TanzaniteOne, KK Security, Keys Hotels, TPC Sugar, Bodi ya Utalii Tanzania, Precisionair na Kilimanjaro Water, kwa kuyafanikisha mashindano hayo ya kila mwaka.

Naye Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema zaidi ya wanariadha 4,000 kutoka nchini zaidi ya 30 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo zikazofanyika Februari, mwakani.

No comments:

Post a Comment