30 November 2010

Polisi yaruhusu mikutano CHADEMA.

Na Tumaini Makene.

SIKU moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kulilalamikia Jeshi la Polisi juu ya kutoa amri ya kuzuia mikutano yake ya hadhara na ile ya kuwapokea wabunge wa
chama hicho maeneo mbalimbali nchini, jeshi hilo limeondoa rasmi zuio hilo.

Jeshi hilo limesema kuwa limeondoa rasmi zuio hilo kuanzia jana baada ya 'uchaguzi kumalizika rasmi juzi' kwa mujibu wa taratibu za ndani za usimamizi wa shughuli ya uchaguzi, ambazo walikuwa wamejiwekea, ambazo hazikuwa zikimlenga mtu wala chama chochote cha siasa.

Jana CHADEMA kilikaririwa na vyombo vya habari kikisema kuwa vitendo hivyo vya polisi vilikuwa vinashiria hatari kwa demokrasia nchini, kuvunja haki za kikatiba na za kisheria za wananchi, huku vikiwa ni dalili ya nchi kupelekwa katika 'dola ya kipolisi,' kama vile ilivyokuwa katika nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini wakati wa utawala wa makaburu na Kenya wakati wa utawala wa Rais wa Pili, Daniel Arap Moi.

Vyombo vya habari vilimnukuu Mkurugenzi wa Haki, Sheria na Katiba wa CHADEMA, Bw. Tundu Lissu akisema kuwa chama hicho hakitakuwa tayari kunyamazia hatua hiyo, kwani ingeweza kuwa mwendelezo wa kuminya haki ya watu kujumuika na kujadili mustakabli wa nchi yao, kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Akizungumza na Majira jana kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, Kamishna wa Polisi Clodwig Mtweve alisema kuwa uzuiaji huo wa maandamano na mikusanyiko ya kuwapokea wabunge na mikutano mingine ya kawaida ya hadhara, ilikuwa sehemu ya utaratibu wa jeshi hilo wakati na baada ya uchaguzi.

Bw. Mtweve alisema kuwa uzuiaji huo haukumlenga mtu yeyote wala chama chochote kile cha siasa, bali ulikuwa ukizingatia hali halisi ya nchi baada ya uchaguzi, ambapo "serikali ilikuwa haijaundwa wala mawaziri hawajateuliwa," hivyo wameondoa rasmi amri hiyo jana.

"Kusema ukweli nimeshaongea na vyombo vya habari vingi leo juu ya suala hilo na nimeshatoa ufafanuzi.  Tulichokuwa tumezuia ni maandamano na kupongezana si mikutano...unajua baada ya bunge kumalizika kulitolewa maombi mbalimbali ya maandamano watu wakitaka kuwapokea wabunge wao.

"Lakini unajua maandamano ni kitu kingine na mikutano ni kitu kingine, kila kimoja kina utaratibu wake, mapema ilikuwa imetolewa amri ya kiutendaji ndani ya Jeshi la Polisi kusimamia mambo yote hayo ya maandamano na mikutano...lakini amri hiyo sasa imeondolewa rasmi leo (jana) baada ya uchaguzi kuisha rasmi jana (juzi)," alisema Bw. Mtweve na kuongeza;

"Kwa mujibu wa utaratibu tuliokuwa tumejiwekea ndani ya jeshi, uchaguzi umemalizika jana (jana)...ma-OCD walipewa maelekezo ya kutoruhusu masuala ya maandamano kwani yale hayaangalii tu kitendo chako cha mwisho, bali yanahusisha taasisi nyingi na masuala ya usalama wa mali za watu, suala hilo halikumlenga mtu wala chama cha siasa...

"Hata hivyo, tulijaribu kuhoji kama ni suala la kupongezana kwani ni lazima watu wapongezane kwa kukusanyika uwanjani, wangeweza kufanya hata hotelini au ukumbini mahali," alisema.

Bw. Mtweve aliongeza kusema kuwa haikuwa vizuri baada ya uchaguzi kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara kwani nchi ilikuwa imetoka katika uchaguzi, huku 'mambo yakiwa hayajakaa sawa', serikali ikiwa haijaundwa na mawaziri hawajateuliwa.

Majira lilipotaka kujua kama jeshi hilo lilikuwa na wasiwasi zaidi na maandamano na mapokezi ya wabunge kwa nini lilizuia hata mikutano ya hadhara kama vile huko Segerea, Dar es Salaam, Bw. Mtweve alisema kuwa hiyo ilikuwa ni kwa mujibu wa "operetion order" (amri ya utendaji).

Alisisitiza kuwa kuanzia jana utaratibu wa kuomba na kukubaliwa mikutano ya hadhara na maandamano unarudi kama kawaida chini ya makamanda wa polisi wa wilaya.

Wakati huo huo, CHADEMA kimepongeza hatua ya kuondoa amri hiyo na kusema kuwa ni jambo zuri lakini halizuii kusudio lake la kufikisha hoja yake bungeni juu ya uvunjifu wa Sheria ya Haki, Mamlaka na Kinga ya Bunge ya mwaka 1988, kikisema kuwa polisi hawana ruhusa ya kuzuia mikutano ya wabunge "pale serikali inapokuwa haipo."

Akipongeza hatua hiyo, Mkurugenzi wa Haki, Sheria na Katiba wa CHADEMA, Bw. Tundu Lissu alisema "Kama wameiondoa basi ni jambo zuri sana...ni kitendo kizuri lakini hakituzuii kwenda kuhoji bungeni kwa nini wabunge wetu walizuia kufanya kazi...kufanya mikutano.

"Hakuna sheria yoyote inayowaruhusu polisi kuvunja au kukiuka sheria ya haki, mamlaka na kinga ya bunge ikiwa serikali haipo au mawaziri hawajateuliwa," alisema Bw. Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni.

5 comments:

  1. NINAWAPONGEZA JESHI LAPOILISI KWA KAZI ZAO NZURI NA ZENYE UMAKINI HAWAKURUPUKI WALA HAWABABAISHWI WANA MSIMAMO NA SABABU ZAO NI ZA MSINGI, BW LISSU NI MWANASHERIA NA ANAJUWA WAKATI WA UCHAGUZI HAKURUHUSIWI MIKUTANO YOTOTE,NI JUZI TU JUMAPILI NDIO UCHAGUZI WA BAADHI YA MAJIMBO UMEMALIZIKA WAMEKOSA SUBIRA. USIWE CHAMA CHA UPINZANI BASI WEWE KILA KITU NI KUPINGA PINGA TUU, HATA KAMA NI KHERI KWA JAMII TUSIJIPENDEKEZE KWA KUJIFANYA MAHODARI SANA WA KILA KITU TUWE WASTAAMILIVU NA WASTAARABU!!

    ReplyDelete
  2. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 30, 2010 at 10:30 AM

    Hongereni sana Jeshi la Polisi kwa kuonyesha ukomavu.Lakini kwanini mseme baada ya kusemwa? Haya tena CHADEMA kumekucha.Kawaambieni wananchi wenu mnawaongoza suala moja kubwa:kwanini mnataka Katiba mpya.Pia waelezeni juu ya ujumbe mliomtumia Rais Kikwete pale Bungeni na maana iliyobebwa na ujumbe ule.Kazi kwenu sasa...hakuna kisingizio chochote hapo!

    ReplyDelete
  3. Nawapongeza Polisi kwa kutambua haraka makosa yao na kuyarekebisha, baada ya CHADEMA kuwafafanulia sheria. Polisi endeleeni kuwa waelewa namna hiyo. kipindi cha uchaguzi kilikamilika baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo. yaliyokuwa yanafuatia ni chaguzi ndogo ambazo zinaweza kufanyika wakati wowote, kwa sehemu husika. kuzuia mikutano na kazi zingine za kisiasa kwa wanasiasa kwa kisingizio cha uchaguzi mdogo unaofanyika katika maeneo machache tu, ni visingizio hafifu visivyo na mashiko. Polisi msitumiwe kuvuruga maslahi ya taifa, kwa visingizio vya kulinda maslahi ya wachache walio madarakani

    ReplyDelete
  4. maofisa wa polisi wanatumiwa na ccm.nyinyi maofisa wa polisi wajinga sana kama hamjasoma vile jutumiwa na wanasiasa wajinga wa ccm wameua nchi.

    ReplyDelete
  5. mchangiaji wa kwanza, umepata wapi hiyo sheria kwamba wakati ya uchaguzi hakuna kufanya mikutano nchini nzima hata mikoa mabayo uchaguzi hakuna na ilishamalizika ??.

    kuhusu kwanini wasifanyie mkutano ndani SIYO KAZI YA POLISI KUWACHAGULIA WATU WAPI WAKAKUTANIE, KAZI YAO NI KUTOA ULINZI KWENYE MIKUTANO HIYO.

    ReplyDelete