*Manji ataka wadhamini waongezeke
Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa Yanga umepanga kumwalika Mdhamini wa klabu hiyo, Yusuf Manji katika kikao cha Kamati ya Utendaji itakayokutana Novemba 23, mwaka huu ili
kuweka wazi maelekezo ya Manji ambayo yamekuwa yakiandikwa na vyombo vya habari nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga alisema wamemwalika Manji ili na yeye aweze kutoa maoni yake ya nini kifanyike kwa ajili ya maendeleo ya Yanga.
Mwenyekiti huyo pia amewahakikishia wanachama wa Yanga kwamba, ndani ya klabu hiyo hakuna mgogoro wowote, hivyo wawe watulivu.
Alisema taarifa zinatoka kwenye vyombo vya habari wengi wanazichukulia tofauti na kuona kama ndani ya Yanga kuna mgogoro kitu ambacho si kweli.
"Nawaomba wanachama wa Yanga wawe watulivu Yanga haina migogoro, ila taarifa zilizokuwa zinatoka wengi walizichukulia vibaya, hivyo nawaombeni muwe watulivu kila kitu kitakwenda sawa," alisema Nchunga.
Aliongeza kwamba uyongozi wao upo wazi kwa kila jambo kama walivyoahidi kabla ya kuingia madarakani, hivyo wanachama watulie na kila kitu wataelezwa.
Katika hatua nyingine, Manji ameuomba uongozi wa klabu hiyo umpe kibali, ili aongeze wadhamini wawili akiwemo Mbunge na mfanyabiashara ili kukamilisha idadi ya wadhamini watano.
Wadhamini waliopo kwa sasa mbali ya Manji ni Fatuma Karume na Francis Kifukwe.
Katika taarifa yake, iliyotolewa mapema wiki hii na gazeti hili kupata nakala yake, Manji alisema anaomba kibali hicho ili itimie idadi ya wadhamini watano katika klabu hiyo, ambao ndiyo wanaotakiwa.
"Nimeomba kibali Yanga, ili niweze kuwatafuta wadhamini wawili kwa ajili ya tutimiza idadi ya wadhamini watano, wadhamini hao mmoja atakuwa Mbunge na mwingine mfanyabiashara," ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Manji.
Aliongeza kuwa anaimani uongozi utafanyia kazi ombi lake, ambalo linalenga kuiletea maendeleo klabu hiyo.
No comments:
Post a Comment