Na Shaban Mbegu
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', Gaudence Mwaikimba amesema atautumia mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya
Kenya 'Harambee Stars' kuonesha kwa nini Kocha Mkuu, Jan Poulsen alimwita katika kikosi hicho.
Kilimanjaro Stars, inatarajiwa kucheza na Harambee Stars Jumatatu kwenye Uwanja wa Uhuru, mchezo ambao ni maalumu kwa timu hiyo inayojiandaa na mashindano ya Chalenji yanayotarajiwa kutimua vumbi Novemba 27, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mwaikimba ambaye ameitwa hivi karibuni na Poulsen, baada ya kuridhika na kiwango chake mara ya mwisho kuzichezea timu za Taifa ilikuwa mwaka 2007, katika kikosi kilichokuwa chini kocha Marcio Maximo aliyemaliza muda wake.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwaikimba alisema tangu alipoitwa tena na kocha huyo, wadau wa michezo nchini wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya uwezo wake, katika kikosi hicho.
Alisema wengi wa mashabiki wa soka walionekana kutokubaliana na kocha huyo, juu kitwa kwake kutokana na kubeza uwezo wake, lakini amejipanga kufanya maajabu katika mchezo huo ili kuwadhihirishia uwezo wake.
"Baada ya kuitwa tena na Poulsen, kuna watu walizungumza mengi sana lakini nimepanga kuwafunga midomo katika mchezo wetu dhidi ya Harambee, na imani Mungu atanisaidia kutimiza lengo langu," alisema Mwaikimba.
No comments:
Post a Comment