25 November 2010

Mgombea CUF amtaka Tendwa kuchukua hatua

Na Gladness Mboma.

ALIYEKUWA Mgombea bunge wa Jimbo la Temeke, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Lucasi Limbu amempa siku tano Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa kuwachukulia
hatua watu wote waliokiuka taratibu za sheria ya uchaguzi wakati wa uchaguzi mkuu.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari jana Dar es Salaam, Bw. Limbu alisema kama Bw. Tendwa hatafanya hivyo atamfikisha mahakamani kwa kutozingatia kazi yake.

Alisema kuwa baada ya kutangazwa kwa sheria hiyo ya uchaguzi, Msajili alionekana kama msimamizi mkuu wa sheria hiyo, pale aliposema kwamba wagombea watakaoshindwa kutii masharti hayo hatasita kuwaengua.

"Yeye (Tendwa) alisema kuwa mkono wake ni mrefu na macho yanaona kila kona, hivyo hatoshindwa kuwachukulia hatua wale wote watakaokwenda kinyume na sheria hiyo," alisema.

Alisema kuwa Temeke hakukuwa na uchaguzi, bali kulikuwa na vurugu na kwamba alitarajia kwamba Bw. Tendwa angechukua hatua haraka iwezekanavyo kutokana na kuvunjwa kwa sheria hiyo, lakini hakufanya hivyo.

Bw. Limbu alisema kuwa pamoja na matatizo yote hayo alipenda sana kuona msajili anasemaje, lakini baada ya uchaguzi kuisha alisema kuwa "uchaguzi umekwisha tugange yajayo" jambo ambalo anadai limemshangaa.

Alisema kuwa anaamini kwamba alishinda katika uchaguzi na sasa yuko katika hatua za mwisho na mwanasheria wake kwa ajili ya kufungua kesi mahakamani.

Bw. Limbu alisema kuwa ana vielelezo vyote vinavyoonyesha kwamba kura zake zilichakachuliwa na kumtaka Bw. Tendwa kutengua matokeo hayo uli mgombea halali aweze kutangazwa bila ya uchaguzi kurudiwa.

Alisema kuwa kama msajili huyo hatochukua hatua hiyo haraka, atambue kuwa katika chaguzi nyingine hakuna atakayefuata sheria hiyo na hapo ndipo machafuko yatakapotokea nchini.

2 comments:

  1. Na Bw. Limbu asipomchukulia hatua Msajili, achukuliwe hatua yeye kwa kulisumbua Gazeti hili na wasomaji wake.

    ReplyDelete
  2. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 25, 2010 at 9:59 AM

    Bwana Limbu hazijui vyema Sheria za Uchaguzi.Utenguaji wa Matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge hufanywa na Mahakama Kuu tu na si Tendwa wala ofisi yake.Tendwa hana lolote...ameshindwa wakati uchaguzi unaendelea ndo ataweza sasa? Sa hizi atamgusa nani? Atathubutuje? Sa hizi ye anajifagilia ili apewe Uteuzi mwingine...anajikosha kwa lami tu. Nasisitiza kuwa usanii wote huu utaishia 2015.

    ReplyDelete