21 November 2010

Kwa hili CHADEMA wana hoja, mfumo wa uchaguzi unachefua .

Na Elisante Kitulo.

HATUA ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kondoka Bungeni wakati Rais Jakya Kikwete alipotoa hotuba ya kuzindua Bunge la 10 mjini Dodoma, imeibua
mjadala na hisia tofauti kwa wananchi.

Ukipita katika mitaa na viunga vya  jiji la Dar es Salaam ni kwa sasa ni kawaida kukuta watu wakijadili hatua hiyo ya CHADEMA ya kususia hotuba ya rais.

Wanasheria na wadau mbalimbali wa masula ya siasa na demokrasia nchini nao wametoa maoni yao kuhusu suala hilo.

Wapo wanaolaani kitendo hicho na kukiita si cha kiungwana,  lakini pia wapo wanaliona suala hilo kuwa la kawaida na linaloashria ukomavu wa demokrasia nchini.

Mwenyekiti wa CHADEMA,Bw. Freeman Mbowe alisema, hatua hiyo ililenga kuujulisha umma wa kimataifa kuwa uchaguzi uliomalizika hivi karibuni haukuwa huru na wa haki.

Alisema kumekuwa na dosari mbalimbali za kiutendaji kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)ambazo zimefanya uchaguzi huo kushindwa kuwa huru na wa haki.

Alisema CHADEMA si kwamba haimtambua Rais Jakaya Kikwete, kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, isipokuwa wanapinga mfumo wa uchaguzi uliomweka madarakani.

Kwa hiyo CHADEMA walilitaka kuwasilisha kwa vitendo kauli yao ya kutotambua matokeo yaliyoweka madarakani serikali iliyopo madarakani.

Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake, Bw. Samuel Sitta alipozungumza na Majira alisema hatua ya wabunge hao kutoka bungeni si kinyume cha Sheria wala Kanuni za Bunge.

Alisema si jambo la kwanza kutokea na kwamba hakuna adhabu yeyote inayoweza kuwapata wabunge hao kwa kuwa wanaruhusiwa kufanya hivyo pasipo kuvunja sheria.

Hali hiyo iliwahi pia kutokea visiwani Zanzibar ambapo Chama Cha Wananchi CUF, hakikuitambua serikali ya Rais Aman Abeid Karume kwa muda.

Wakati haya yakijiri tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa tamko la kulaani kitendo cha wabunge hao wa CHADEMA.

Niliwahi kuandika na kusema kuwa chaguzi za Tanzania zitaendelea kughubikwa na malalamiko kila wakati iwapo jitihada zinazolenga kuufanya marekebisho katika mfumo wa uchaguzi hazitafanyika.

Nilisema,haki haipaswi tu kutendeka bali inapaswa kuonekana imetendeka na ili hilo litokee , NEC inapaswa kuwa chombo huru, isiyotokana na uteuzi wa serikali iliyopo madarakani.

Hatua ya wabunge wa chadema kutoka bungeni wakati rais anahutubia Bunge la 10 mjini Dodoma Alhamisi wiki hii,haipaswi tu kupuuzwa bali ichukuliwe kama changamoto kuboresha mfumo wa uchaguzi nchini.

Ikumbukwe kuwa, CHADEMA, si kwamba haimtambui Rais kikwete kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, bali inapinga mfumo wa uchaguzi uliomweka madarakani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Jakaya Kikwete ni rais halali  wa nchi hii, jambo ambalo CHADEMA wanalikubali isipokuwa wanapinga utaratibu uliomweka madarakani.

Ikumbukwe kwamba malalamiko ya CHADEMA yalianza mapema wakati tume hiyo ilipoanza kutangaza matokeo ya urais kwa baadhi ya majimbo na kuiomba tume hiyo isitishe kuyatangaza ili ijiridhishe kwanza uwiano wa matokeo hayo kama yalivyo majimboni.

Ni muhimu kutambua kuwa, ni rahisi kukubali matokeo ya ubunge kwa kuwa yanahesabiwa majimboni na yanaweza kupingwa mahakamani.

Lakini kwa upande wa matokeo ya urais, pindi yanapotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi, hayawezi kupingwa katika mamlaka yeyote.

Kwa mujibu wa katiba,haijalishi nani kashinda kwenye kura, bali nani katangazwa mshindi na mamlaka iliyopewa dhamana ya kutangaza matokeo ya urais.

Hili ni tatizo jingine la kikatiba, ambalo wanaharakati na wadau wa demokrasia nchini wamekuwa wakipaza sauti kudai marekebisho ya kikatiba, yatakayoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Hivyo suala ya wabunge wa CHADEMA kufikia hatu hiyo linatokana na mapungufu ya kisheria yanayoufanya mfumo wetu wa uchaguzi kuonekana hakutotenda haki.

Tanzania inasifika kuwa nchi ya amani na utulivu kwa muda mrefu kutokana na misingi imara ya umoja na upendo iliyowekwa na waasisi wa taifa hili.

Ili sifa hiyo iendelee kuwa yetu, tunapaswa kuchukua hatua za makusudi za kuziba nyufa zinazo hatarisha umoja wa kitaifa.

Machafuko mengi ulimwenguni yanatokana na maumivu ya muda mrefu ya kisiasa jambo ambalo huibua chuki na uhasama.

Tusiwahukumu tu kwa kitendo hicho, bali tuende mbele zaidi na kutafakari kiini cha matatizo yalisababisha wafikie hatu hiyo na kuona namna ya kuyapatia ufumbuzi.

Madai ya CHADEMA yanawakilisha kundi kubwa la watu wenye makovu ya kisiasa ambao wamekuwa walalamikia mfumo wa uchaguzi na kudai ufanyiwe marekebisho.

Tukipuuza madai ya CHADEMA leo,ambayo naamini  si wa kwanza kulalamikia mfumo wa uchaguzi,tutawagawa watanzania jambo ambalo nisingependa litokee.

Naamini mabadiliko ya Kisheria na Muundo wa mfumo mzima wa uchaguzi yanaweza kufanyika ili haki ionekane kutendeka katika chaguzi zijazo.

Naamini pia kuwa ujumbe walioukusudia kuutoa wabunge hao, umefika kwa wahusika, wazike tofauti hizo na kuwatumikia wananchi waliowachagua.

1 comment:

  1. mbowe kaza uzi, usimsikilize mrema au maalim self, hao tako zamani ni ccm damu na nia yao kubwa si kuwakomboa watanzania bali ni kulilia madaraka, rejea mrema akimkampenia kikwete badala ya mgombea wa chama chake ingawa yeye ni mwenyekiti wa chama hicho NA AKIOMBA APEWE UWAZIRI WA MAMBO YA NDANI, au maalim self yeye ameshapewa umakam na sare ya suti ya ccm, sasa anaona eti kumgomea rais kikwete ni UHAINI!!JAMANI SIASA WEWE MAALIM SELF HATA UNAKUJA DAR UNAFIKIA IKILU HATA BILA KUFIKA BUGURUNI KUONANA NA NDUGU YAKO LIPUMBA!!!UMESAHAU JINSI WANA CUF WALIVOPIGWA RISASI!!
    KATIBA MPYA, TUME HURU YA UCHAGUZI NI LAZIMA,

    ReplyDelete