16 November 2010

Kipingu ampa changamoto Jaji Mkuu.

Na Amina Athumani

MWENYEKITI wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu amemtaka mlezi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), ambaye pia ni Jaji Mkuu
wa Tanzania Agustino Ramadhani, kuhakikisha anatumia nafasi yake kuukuza mchezo huo ili uweze kupiga hatua ya kimaendeleo.

Kipingu aliyasema hayo Dar es Salaam wakati, akiiaga timu ya taifa ya taifa ya kikapu ya Komoro, ambayo ilikuja nchini kucheza mbili za kirafiki na Tanzania ambayo jana iliondoka kurudi kwao.

Kipingu pia aliipongeza timu ya Tanzania kwa kuonesha mchezo mzuri juzi, baada ya kuifunga Komoro katika mchezo wa marudiano kwa pointi 57-51, wakati awali Komoro iliifunga Tanzania kwa pointi 65-55.

"Tunawashukuru sana kwa kufika kwenu nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutoa changamotto kwa timu yetu kwani mmeweza kuiamsha na kuichangamsha, pia tunawakaribisha tena kuja nchini kwa ajili ya kucheza mchezo mwingine kama huu," alisema Kipingu.

Alisema kwa nafasi yake katika baraza ya kuhakikisha michezo inakuwa kwa kiasi kikubwa, atakuwa bega kwa bega na serikali ili kuona mpira wa kikapu unapewa kipaumbele kwa kuwa ni mchezo unaoweza kuiletea heshima kubwa nchi, kama ilivyokuwa kwa mchezaji Hashim Thabit, anayechezea timu ya Memphees inayoshiriki Ligi Kuu ya kikapu nchini Marekani (NBA).

Naye Jaji Ramadhani aliiahidi Komoro kuwa timu ya Tanzania itawasili nchini kwao kwa ajili ya mchezo wa kirafiki, huku akiahidi yeye kuwa atakuwa mkuu wa msafara.

"Tunawaahidi tutashirikiana na TBF Kuhakikisha timu ya Tanzania inakuja nchini Komoro kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki, ili tuweze kudumisha umoja na ushirikiano ambao tumeuweka baina yetu na ninyi," alisema Jaji Ramadhani.

No comments:

Post a Comment