16 November 2010

Hatutakubali kuteuliwa na Kikwete-CHADEMA.

Na Peter Saramba, Dodoma

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa msimamo kuwa hakitakubali kushirikishwa kwenye baraza la mawaziri litakaloundwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hata
kama watateuliwa, kwa sababu hakiamini wala kutambua matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa hoteli ya Desert Pub Resort mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema chama chake hakitakubali wala kupokea uteuzi wa nafasi ya uwaziri hata kama Rais Kikwete ataamua kumteua mbunge yeyote kutoka chama hicho katika nafasi ya uwaziri.

"Hatuko CHADEMA wala kuingia bungeni kutafuta uwaziri. Siku zote lengo letu ni kusimamia na kupigania haki ya Watanzania kwa kutumia njia sahihi na halali kwa kushinikiza serikali kuongoza kwa kujibu wa mahitaji ya umma. Hatuko hapa (ndani ya chama) kutafuta kushirikishwa kwenye serikali ya CCM.

Tunalenga kueneza sera zetu kwa wananchi na hatimaye kuongoza dola siku zijazo kwa kuungwa mkono na Watanzania kupitia sanduku la kura," alisema Bw. Mbowe katika mkutano ambao mgombea urais wa chama hicho, Dkt. Willibrod Slaa alieleza msimamo wake.

Mwenyekiti huyo aliyekuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi aliyetaka kujua iwapo watakubali uteuzi kwenye nafasi ya uwaziri wakati hawatambui ushindi wa Rais Kikwete, alisema wabunge na madiwani wa chama chake watashirikiana na mamlaka zilizopo
kutekeleza majukumu yao kisheria huku wakiendeleza shinikizo la kuwepo mabadiliko katika mfumo wa sheria, katiba na uongozi kwa ujumla.

"Tutakachofanya kama chama cha siasa makini kinachokusudia kushika dola ni kutekeleza majukumu yetu kulingana na sheria mbaya zilizopo huku tukiweka msimamo wetu wazi kuwa hatujaridhika na wala hatutaridhika na namna chaguzi zetu zinavyoendeshwa," alisema Bw. Mbowe.

Akifafanua, alisema kisheria Rais Kikwete ni kiongozi halali wa nchi na hakuna chombo wala mamlaka ya kuhoji au kubatilisha matokeo yaliyompa ushindi hata kama kuna ushahidi wa kuwepo kasoro nyingi katika mchakato wa uchaguzi na utangazaji wa matokea ya kura zilizompa ushindi huo.

Aliwaasa wananchi kote nchini kuiunga mkono CHADEMA katika harakati za kudai uongozi unaojibu mahitaji ya umma badala ya hali ilivyo sasa ambapo viongozi wa chama tawala wanajali zaidi maslahi ya chama chao na kundi dogo la watu wanaotafuna raslimali za nchi kwa njia zisizofaa.

Bw. Mbowe aliahidi kuwa chama chake kitafuata na kuzingatia sheria na katiba katika kutekeleza majukumu yake huku kikiweka kipaumbele kwenye usalama wa nchi, umoja na mshikamano katika jamii na kuwataka wanachama na wapenzi wa CHADEMA kuepuka mambo yote yanayoweza kuhatarisha usalama wao na nchi kwa ujumla.

6 comments:

  1. pETRO eUSEBIUS mSELEWANovember 16, 2010 at 10:36 AM

    Mwandishi aliyemuuliza Mh.Mbowe hajui vizuri utaratibu wa utawala nchi yetu.Hata kama Ibara za 54 na 55 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977 ziko kimya juu ya vyama wanavyopasa kutoka Mawaziri na Manaibu wao,hakuna hata siku moja ambapo hao wamewahi kuteuliwa kutoka vyama vya upinzani.Hii haijawahi tokea.Labda,Katiba yetu ikifanyiwa mabadiliko.Kwa Nchi hii na utawala wa Chama hiki,mabadiliko hayo hayako hata njiani...labda ndo kwanza yanaoga.

    ReplyDelete
  2. INASHANGAZA SANA KUONA VIONGOZI WALIOKUWA WANATEGEMEWA NA HAO WANA CHADEMA WANAJIBU UTUMBO!!WANADAI HAWAMTAMBUI RAISI WALA UTEUZI WAKE WA BARAZA LA MAWAZIRI,NI UNAFIKI SASA YEYE KAPEWA KUWA KIONGOZI WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI ATAWAJIBIKA KUJIBU HOJA ZA MAWAZIRI HALALI WA SERIKALI KAMA WAO NI MAWAZIRI VIVULI WATAWAJIBIKAJE WAKATI HOJA ZA HAO MAWAZIRI HAWAWATAMBUI? WANADAI HAWANA HAJA YA UWAZIRI NADHANI NIA YAO NI URAISI NA WALIJIPA MOYO KUWA HUYO MPIGANAJI(SILAHA) ATAPATA HAWA JAMAA WAMEJIPANGA ZAMANI KA VURUGU NA NDIO HATA MAVAZI YAO NI MAGWANDA KAMA ASKARI WA JIJI AU MGAMBO INASIKITISHA SANA TENA SASA NDIO TUNAPATA PICHA KAMILI YA UBORA WAO KUMBE NI MATATIZO TUU SI WAUNGWANA NA NI WENYE UCHU WA MADARAKA

    ReplyDelete
  3. Hujui sheria hustahili kuchangia. Kwa taarifa yako tu; Rais JK hatambuliki na serikali vivuli zitaundwa; najua inakuuma sana ila ni umaskini wa akili ndio unakufanya upige mayowe. Na bado rais wenu atakuwa anaongea peke yake njiani; binafsi simtambui; ingeruhusiwa kuchangia PAYE yangu sehemu nyingine ningeitoa ktk serikali ya JK; very tired

    PEOPLES POWERRRRRRRRRRRRRR!!!!

    ReplyDelete
  4. Huyu vipi? kwani aliambiwa chadema watapewa uwaziri? kwa kuwa? sahau hizo ni ndoto za mchana, JK hata hafikirii kukutieni ktk cabinet yake! hayo ni maruweruwe yenu tu, msipomtambua mkimtabua yeye ndio RAIS!

    ReplyDelete
  5. CHADEMA KUWENI WASTAARABU NA MFIKILIE MBALI KWANI KAMA HAMUMTAMBUI RAIS NA MAWAZIRI WAKE MNAKWENDA BUNGENI KUFANYA NINI?KAMA KWELI NYIE MNAWAKILISHA WANANCHI WENU MTAIOJI VIPI SERIKALI KUHUSU MAENDELEO YA MAJIMBO YENU?

    KWELI NYIE MNAO UCHU WA MADARAKA

    ReplyDelete
  6. Jamani watanzania wenzangu tusijichanganye. Chadema hamuwezi kututangazia kuwa hamtambui rais bila kutupa vielelezo vyenu kuonyesha wizi. Mnasema mtavitoa baadaye, kwanini hamkuvitoa kabla hajaapishwa? kulikuwa na muda wa kutosha. Au mlikuwa hamjamaliza kuvichakachua. Sababu kama mna vielelezo na mnaamini vilikuwa sahihi mngevitoa kwa watanzania siku ile mlipoiambia tume isitishe kuhesabu kura. Sasa rais ametangazwa, ameapishwa, spika kachaguliwa, waziri mkuu ameteuliwa, nyie bado mnalia mna vielelezo na mtavitoa kwa faida ya nani. Hiyo process imepita afadhali mmeze hivyo vielelezo vyenu jiandaeni kwa 2015. Bado mna kazi kubwa ya kujenga chama chenu. CCM imejijenga kwa muda mrefu hamuiwezi. Msije mkadhani mmekwishafikia level ya CCM, ndiyo maana mmepoteza uchaguzi. CCM ilikuwa haina haja ya kuiba kura. Hata kura za maoni zilitabiri matokeo haya, kuwa kikwete atashinda na upinzani utapata viti zaidi vya ubunge. Msiendelee kuwachanganya watanzania. Mkiedelea kucheza uanasesere mnaofanya sasa hivi watanzania watawazarau na hii hatua mliyopiga katika uchaguzi huu itapotea mkajikuta hata namba ya wabunge mliyoipata 2015 ikapotea. Hei guys grow up, kuna kazi kubwa ya kufanya bungeni. Kutomtambua rais siyo maslahi kwa taifa.

    ReplyDelete