27 October 2010

Yanga, Simba kazi moja leo.

Na Zahoro Mlanzi
MSHIKEMSHIKE wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, leo unaendelea kwa kupigwa michezo minne katika viwanja tofauti, huku macho na masikio ya mashabiki yakiwa kwa timu kongwe za
Yanga na Simba, zitakapokuwa vinywani mwa African Lyon na Kagera Sugar.

Vinara wa ligi hiyo, Yanga watakuwa ugenini Mkoani Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri kwa kuumana na Lyon katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani.

Katika mchezo huo, Yanga haitakubali kupoteza kwani itakapokubali kufungwa, itakuwa imeipa Simba nafasi ya kuongoza endapo nayo itashinda mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, utakaopigwa Mkoani Kagera, kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Timu hizo kwa sasa zinawiana kwa pointi zote zikiwa na pointi 21, ila zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa ambapo, Yanga ina uwiano mzuri ikiwa na mabao tisa na Simba mabao saba.

Lyon na Yanga zilipokutana msimu uliopita katika mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya bao 1-1, ambapo bao la Yanga lilifungwa na Jerson Tegete na la Lyon, lilifungwa na Rashid Gumbo na mzunguko wa pili Lyon ikafungwa 2-0 kwa mabao ya Tegete na Mrisho Ngassa, ambaye kwa sasa yupo Azam FC.

Kocha wa Yanga, Kostadin Papic ambaye kwa hivi karibuni amekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa timu yake kutoka sare mara mbili mfululizo, atakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha inashinda katika mchezo huo.

Kwa upande wa Simba, pia itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Kagera Sugar, kwani msimu uliopita, Simba ilipata pointi moja kwenye uwanja huo kwa kutoka sare ya bao 1-1, bao la Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi na la Kagera, likafungwa na Themi Felix.

Lakini huo ulikuwa ni mzunguko wa pili, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mzunguko wa kwanza Simba, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Haruna Moshi 'Boban' na Mohamed Kijuso.

Kocha wa Simba, Patrick Phiri ametamba kuendeleza kasi aliyoianza kwani kikubwa anachotaka ni kuona timu yake inakuwa kileleni na kutetea ubingwa kwa mara nyingine.

Michezo mingine itapigwa jijini Mwanza na Mkoani Morogoro, ambapo wenyeji Toto African itaikaribisha Majimaji ya Songea na Uwanja wa Manungu, Mtibwa Sugar itaumana na AFC ya Arusha.

Toto ipo nafasi ya saba kwa pointi 12, endapo itashinda na Kagera na Mtibwa zikafungwa, itapanda mpaka nafasi ya tatu kwani Kagera na Mtibwa zitabaki na pointi zao 14.

Wakati Toto ikiziombea mabaya timu hizo, AFC wao watakuwa na furaha endapo dua hizo zitakuwa za kweli, kwani itakuwa imepata ushindi wa pili katika michezo tisa na itafikisha pointi saba, sawa na Ruvu Shooting na Majimaji lakini endapo kama Majimaji itapoteza.

No comments:

Post a Comment