Na Grace Michael
KESI ya kikatiba inayopinga sheria inayozuia kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais inatarajiwa kutajwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania siku moja baada ya uchaguzi mkuu
kufanyika, tofauti na matarajio ya mwombaji katika kesi hiyo.
Hatua hiyo ilijulikana jana mahakamani hapo mbele ya majaji Ibrahim Juma na Faudhi Twaib wakati kesi hiyo ilipotajwa, ambapo mdai, Bw. Denis Maringo aliomba mahakama kutoa uamuzi wa maombi hayo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.
Hata hivyo, ndoto ya mwombaji huyo ilipotea baada ya mahakama hiyo kuupangia upande wa serikali kuwasilisha majibu yake Oktoba 29, mwaka huu na kutajwa Novemba 1, mwaka huu baada ya kufanyika kwa uchaguzi.
Katika kesi hiyo, Bw. Maringo anapinga sheria inayozuia matokeo ya uchaguzi wa rais yakishatangazwa kupingwa katika chombo chochote.
Bw. Maringo alilazimika kuieleza mahakama kuwa endapo uamuzi utatolewa baada ya uchaguzi utakuwa hauna maana kwa kuwa alifungua kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu.
“Kama kesi hii itatajwa Novemba 1, mwaka huu basi itakuwa haina maana kwani tumefungua kwa ajili ya kupinga sheria hiyo na kupinga taratibu mbovu za uchaguzi,†alidai Bw. Maringo.
Hata hivyo, majaji walilazimika kumhoji kuwa “unaposema ulifungua kesi ili itolewe uamuzi kabla ya uchaguzi kwa nini ulichelewa kuifungua kwani tangu Januari mwaka huu si ulifahamu kuwa uchaguzi wa Tanzania utafanyika,†alihoji Jaji Juma.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Maringo alielezwa kuwa kama hajaridhika na namna mahakama hiyo ilivyopanga basi afuate utaratibu mwingine wa kisheria wa kupinga uamuzi huo.
Katika kesi hiyo, upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bi. Alesia Mbuya na mdai alijiwakilisha mwenyewe.
Kesi hiyo namba 86/2010 ilifunguliwa mahakamani hapo Oktoba 11, mwaka huu na Bw. Maringo pamoja na Kituo cha Haki na Demokrasia dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
No comments:
Post a Comment