Na Suleiman Abeid, Shinyanga
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora,
imewahukumu washtakiwa sita adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuwatia
hatiani katika makosa ya kuua kwa kukusudia.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Simon Lukelelwa aliyekuwa
akisikiliza kesi nne tofauti zilizohusu mauaji ya kikatili ambayo yamefanywa
kwa wanawake vikongwe kutokana na imani potofu za kishirikina.
Mauaji hayo yalifanyika kati ya 2005 na 2007 katika Wilaya za
Shinyanga, Kahama na Bukombe ambako wanawake vikongwe wanne, waliuawa kikatili
kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao hadi kufa.
Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Venance Nuba na Tegemeo Paulo ambao
walitiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Sophia Gundu, Januari 25,
2006, Kijiji cha Kazibizyo, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
Washtakiwa wengine waliokumbwa na adhabu hiyo
ni Joseph Lushika na Maziku Mpigachai waliotiwa hatiani kwa kosa la kumuua kwa
kukusudia Monica Bulemela, Mei 6, 2005, katika Kijiji cha Bulembela, wilayani
Bukombe.
Mshtakiwa mwingine ni Mhande Manyanya
aliyeshtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia mkazi wa Kijiji cha Ihapa,
Wilaya ya Shinyanga, Wande Bulugu, Julai mosi 2007,Kijiji cha Ihapa.
Jaji Lukelelwa pia
alitoa hukumu kama hiyo kwa mshtakiwa Tembo
Hussein, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuwa
mshtakiwa alimuua kwa kukusudia Anjelina Hungwi, mkazi wa Kijiji cha Itega,
wilayani Kahama.
No comments:
Post a Comment