Rais Jakaya Kikwete(kulia), akisalimiana na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA),Bw. Tundu Lissu baada ya kuwasili Ikulu, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mbunge wa Kuteuliwa kwa tiketi ya Chama cha NCCR- Mageuzi, Bw.James Mbatia. Viongozi wa vyama hivyo na CUF, walikwenda Ikulu kufanya mazungumzo na Rais Kikwete juu ya mchakato wa Katiba Mpya.
- WAMUANGUKIA RAIS KIKWETE ASISAINI MUSWADA WA KATIBA
Na Eckland
Mwaffisi
Rais Jakaya Kikwete, jana alikutana na viongozi wa vyama vya siasa
vyenye uwakilishi bungeni ili kujadili maendeleo ya mchakato wa Katiba Mpya
nchini.
Viongozi hao
waliokutana Ikulu, Dar es Salaam
ambao ni Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ndiye
msemaji wa viongozi hao, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe na Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia.
Wengine ni
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bw. Philip Mangula, Bw. Isaack Cheyo aliyemwakilisha
Mwenyekiti wa Chama cha UDP, Bw. John Cheyo na na Mrindoko ambaye alimwakilisha
Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Bw. Augustine Mrema.
Taarifa
iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema Bw. Cheyo na
Bw. Mrema wako nje ya nchi. Kurugenzi hiyo iliongeza kuwa, viongozi wengine
waliokuwepo katika mazungumzo na Rais Kikwete ni Bw. Habib Mnyaa, Bw. Julius
Mtatiro wote kutoka CUF, Bw. Tundu Lissu, Bw. John Mnyika kutoka CHADEMA na Bw.
Martin Mng'ongo wa NCCR-Mageuzi.
Rais Kikwete alikutana na viongozi hao ili
kuondoa sintofahamu iliyopo kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba 2013, uliopitishwa na Bunge, Mjini Dodoma, hivi
karibuni.
Maazimio ya kikao
Vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na
mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
viwasilishe mapendekezo yao
haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kushirikisha mapendekezo hayo katika
marekebisho ya Sheria.
Pili vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya,
viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano, maridhiano ili
kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi na mustakabali wa
taifa.
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimepewa
jukumu la kuratibu jambo hilo
pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.
Katika waraka wao kwa Rais Kikwete, vyama
hivyo vilimshauri atumie mamlaka aliyonayo chini ya ibara ya 97(2) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano kutoukubali Muswada huo kwani sheria hiyo inasubiri ridhaa
yake kabla ya kuanza kutumika.
Waraka huo uliongeza kuwa, ushauri huo
unatokana na imani yao kwamba, kama muswada huo utapata ridhaa yake na kuanza
kutumika kama Sheria, utakuwa na madhara makubwa kwa mchakato mzima wa utungaji
Katiba Mpya, kwa amani na utulivu wa nchi.
Katika waraka huo, vyama hivyo vilisema
Muswada umefanya marekebisho makubwa katika namna ya kupitisha vifungu vya
Katiba Mpya katika Bunge Maalum la Katiba.
Wakati kifungu cha 26(2) cha Sheria kama
ilivyo sasa kinalazimu ili Katiba Mpya ipitishwe, sharti ikubaliwe na theluthi
mbili ya wajumbe wote wa kutoka Tanganyika
na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar na
marekebisho yaliyofanywa kwenye Muswada huu yameondoa sharti hilo.
Kama theluthi mbili haitapatikana ndani ya
Bunge Maalum la Katiba baada ya kupiga kura mara mbili, Katiba Mpya itapitishwa
kwa wingi wa kawaida wa wajumbe wote wa Tanganyika
na idadi hiyo hiyo ya wajumbe kutoka Zanzibar.
"Muswada huu ni mojawapo ya Muswada wa
aina ya pili, yaani, Muswada ambao haukufanyiwa tafakuri ya kutosha na
kuzingatia masilahi mapana ya kupata Katiba Mpya ya nchi yetu kwa njia ya
mwafaka wa kitaifa na maridhiano ya wadau wote.
"Muswada huu hautajenga maelewano kuhusu
namna ya kutatua matatizo ya Muungano wetu, wala hautaziba nyufa zilizojengwa
katika mchakato huu.
"Badala
ya kutuunganisha, Muswada huu utatugawa zaidi badala ya kutibu majeraha yetu ya
kisiasa na kijamii, Muswada huu utayawekea chumvi na kuyafanya yawe makubwa
zaidi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment