Na Mwandishi Wetu
Wakati zikiwa zimebaki siku tatu
watani wa jadi, Simba na Yanga washuke dimbani wachezaji na mashabiki wa timu
hizo mioyo imekuwa ikidunda kutokana na presha ya mchezo huo.
Wakongwe hao wa soka
nchini, wanatarajia kushuka uwanjani Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu
itakayochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam unaochukua watu 57.
Katika msimamo wa ligi
hiyo, Simba wanaongoza wakiwa na pointi 18 wakiwa hawajafungwa mechi hata moja
huku watani wao Yanga, wakishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15 wakiwa
wamefungwa mechi moja dhidi ya Azam FC.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti mashabiki wa timu hizo, wanaopenda kukaa makao makuu ya klabu hizo Mtaa
wa Msimbazi kwa Simba na Twiga na Jangwani kwa upande wa Yanga, mashabiki hao
kila mmoja ametamba timu yake kuibuka na ushindi.
Akizungumza kwa niaba ya mashabiki wenzake waliomzunguka katika makao ya
Klabu ya Simba, mmoja wa mashabiki hao aliyejitambulisha kwa jina la Chaurembo
Ally, alisema ana uhakika na timu yake ya msimu huu tofauti na msimu uliopita.
"Msimu huu tuna timu nzuri ndiyo maana
tuna imani kubwa na mechi hii, tuna washambuliaji wazuri na wenye uchu na pia
viungo na mabeki tuna imani nao kubwa hivyo Jumamosi, tunakwenda uwanjani
kuongeza pointi tatu muhimu.
Huku Tamba (Amis), huku Mombeki (Betram) na pale Kiemba (Amri), hapa
Chanongo... wamekwisha Yanga, hii si Simba ile waliyoizoea bwana,"
alitamba shabiki huyo huku akishangiliwa na wenzake.
Alisema mwaka huu watatangaza ubingwa mapema kutokana na ubora wa kikosi
chao kinachotengenezwa na makocha wazawa, Abdallah 'King' Kibadeni ambaye ni
Kocha Mkuu akisaidiwa na Jamhuri Kihwelo 'Julio'.
Nao mashabiki wa Yanga kwa upande wao, wametamba kwamba Jumamosi hatumwi
mtoto sokoni kwa kuwa wana kikosi imara, hivyo Simba wasubiri kipigo.
Akizungumza kwa niaba ya mashabiki wenzake, Athuman Libaba alisema licha
ya kwamba Simba wanaongoza ligi watahakikisha kipigo cha kwanza wanakumbana
nacho Jumamosi.
"Ndugu mwandishi sisi hatuna
maneno mengi, sisi kazi yetu ni vitendo tu njoo Jumamosi utaona shughuli yetu,
we ukiona manyoya tu ujue kaliwa huyo," alitamba Libaba.
No comments:
Post a Comment