Leah Daudi na Fatuma Mshamu
Maendeleo ya afya ya mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro,
yameendelea kuwa siri yake na madaktari wanaomtibu hadi siku tatu zijazo ambapo
ataruhusiwa kuonana na watu wanaotaka kumjulia hali.Hata hivyo
habari zinaeleza kuwa hali ya mwandishi huyo imezidi kuimarika.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Aminiel Aligaisha, alisema kwa mujibu wa daktari anayemtibu hali yake
inaendelea vizuri, lakini hakuna ruhusa ya mtu kwenda kumuona kwani kwa sasa
yupo katika mapumziko ya siku tatu.
"Hali
yake inaendelea vizuri kutokana na maelezo ya daktari wake anayempatia
matibabu, hivyo ni fursa yetu kuweza kumuombea ili aweze kupona," alisema.
Alisema Saro
alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili katika wodi ya Kibasila na baadaye
kuhamishiwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Alisema kuwa kwa sasa, Saro amelazwa katika
jengo la matibabu ya moyo na yupo katika wodi za wagonjwa wa kawaida ambapo
tangu jana (juzi) hali yake iliendelea kuimarika na jana asubuhi aliweza
kuzungumza na daktari wake.
Wakati huo huo, mwili wa mama yake, Anastazia Peter Saro, umeagwa jana katika
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania,
Ushariki wa Kibwegere Kibamba na kusafirishwa kwenda kijijini kwake Shari, Machame mkoani Moshi kwa mazishi ambayo
yatafanyika leo.
Bi Saro
alijeruhiwa Oktoba 13 kwa risasi na mzazi mwenzake, Anter Mushi, ambapo katika
tukio hilo alimuua mama mkwe wake (Anastazia) na yeye kujipiga risasi ya
kidevuni iliyotokea kichwani na kusababisha kifo chake.Mushi alikuwa akifanya
kazi katika ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini Darfur nchini Sudan
No comments:
Post a Comment