17 October 2013

RAIS KIKWETE YUPO SAHIHI KUSAINI MSWADA WA KATIBA



Hamisi Kigwangalla

  Kama ningemshauri Rais Jakaya Kikwete hata kidogo tu kwenye hili la Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, ningemshauri aisaini sheria hiyo.

Ushauri wangu unazingatia lengo moja kubwa la kutengeneza mwafaka wa kitaifa na kwa maana hiyo makundi yote ndani na nje ya Bunge ni muhimu ili afanikishe kutupatia lengo hilo.
  Pia, ili kupata mwafaka na kundi moja ni busara kulinda ulichonacho mkononi kabla ya kile kilicho angani, kama wanavyosema wazungu kwenye semi zao kuwa one bird in hand is worth more than a thousand on a tree,
(unayotafsirika kama ndege mmoja mkononi ana thamani kubwa zaidi ya elfu moja mtini! ).
  Tayari Rais Kikwete, kama mkuu wa nchi, anakuwa na jukumu la kimaadili na la kiuongozi kuhakikisha anatufikisha salama kama Watanzania kwenye mchakato huu. Hatumtegemei asiwasikilize wapinzani na wadau wengine wote, hapana. Kuwasikiliza ndiyo uongozi.
  Ni lazima awasikilize wote na atafute usawa kwenye mizania ya haki ili kuwe na mwafaka wa kitaifa kwenye zoezi hili nyeti. Na binafsi nichukue fursa hii kumpongeza kwa kuwa msikivu, mvumilivu na mwenye kujenga madaraja na watu wote, badala ya uzio wa ukuta.
  Kufanikisha mchakato wa kuandika katiba linapaswa kuwa jukumu la kwanza la kimaadili la Watanzania wote tunaoishi leo.

   Kwa viongozi wote hii ni dhamana kubwa kwao. Kuwa makini na waangalifu, kuwa na maadili ya kiuongozi na wakweli wakati wote, kuwa wavumilivu na wenye subira kwa wenzetu ni tabia ambazo zitatufi kisha salama hivyo tuzikumbatie.
  Hivi karibuni Rais Kikwete, akilihutubia taifa, pamoja na mambo mengine alizungumzia sintofahamu iliyojitokeza kwenye mchakato wa majadiliano na hatimaye kupitishwa kwa Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.
Mkuu wa Nchi, pamoja na kufafanua mambo mengine alisema Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. 
  Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi mwafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa
  Mswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa. Dkt. Kikwete, katika hotuba yake alishauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze. Mimi nimejiuliza tu kuwa linarudi katika sura ipi? Na je kurudi inamaanisha nini? Kwamba,mchakato ulikosewa japokuwa Rais anaweka wazi kwenye hotuba yake kuwa haukukosewa. Sasa kwa nini tunarudi nyuma jibu hapo ni moja tu kuwa tunatafuta mwafaka wa kitaifa wa kutupeleka kupata katiba mpya.
  Hili ni lengo la kila mwenye akili timamu. Nalikubali na nampongeza Rais wetu kwa uamuzi huu mzuri. Je, kurudi inamaanisha tunaanza upya ama
tunaanzia wapi? Hoja ya makala yangu ni kushauri namna gani suala hili linarudi bungeni na linarudi kwa mwafaka wa kitaifa ambao ni nia ya wazi ya Rais, kwa mujibu wa hotuba yake.
  Kwa kuwa hoja ya mswada huu ilipitia hatua zote za lazima za kikanuni na kwa kuwa kuna kundi la wabunge walishiriki kikamilifu hata kufi kia mswada ule kupita na kwa kuwa imebakia sehemu moja ya Bunge tu kukamilisha kazi ya kutunga sheria, ambayo ni Rais,ushauri wangu ni kuwa Rais aisaini kwa faida ya kuondoa uwezekano wowote ule wa kutengeneza matabaka ya wabunge walio wengi (majority) kutokufurahishwa na hatua hiyo, kwa kitu ambacho wanaamini kilikuwa sahihi na kiliiva ipasavyo.
  Pili, kwa kuwa kulikuwa na wabunge walio wachache bungeni (minority) na kwa kuwa katika demokrasia yoyote ile yenye afya nzuri maoni na sauti za wachache ni lazima yasikilizwe kwa umakini zaidi hata ya wale walio wengi; na kwa kuwa kupitishwa kwa sheria ile haimaanishi kuwa ni lazima ilikuwa sahihi kwa asilimia 100; na kwa kuwa tayari Rais amechukua jukumu lake la kiuongozi la kuliunganisha tena Bunge letu, ili liwe na sura ya umoja na mshikamano wa kitaifa, ni busara kurudi mezani na kusikilizana na kisha kuleta mapendekezo ya vipengele vinavyowakosesha usingizi na amani wapinzania kwa njia ya muswada wa mabadiliko ya sheria (ambayo itakuwa imekwishasainiwa sasa na Rais).
  Kuna swali litahitaji majibu kama uamuzi wa kuchukuwa njia inayoendana na ushauri wangu itafuatwa. Kwamba, ni namna gani tutarudi kuchukuwa maoni ya Wazanzibari, yanayolalamikiwa na wapinzani, ilhali sheria itakuwa imeishasainiwa na kutakuwa kumeletwa vifungu tu vinavyohitaji kufanyiwa marekebisho?
  Maoni yatakuwa kwenye vifungu hivyo tu ama kwenye Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 yote? Na kama Rais akiamua kufuata njia nyingine na pekee iliyopo, nje ya hii ninayoipendekeza mimi, ni kuacha kusaini Sheria hii iliyokwisha kupitishwa. Kama akifuata njia hii kuna mambo mawili yanaweza kutokea; kununa kwa wabunge walio wengi na walioipitisha na kuharibika kwa ratiba nzima ya mchakato wa katiba,maana ifahamike wazi hapa kuwa bila kuwepo kwa sheria hii, Bunge la katiba halitoweza kuitishwa.
  Madhara ya kuvurugika kwa ratiba ya mchakato wa katiba ni pamoja na kuchelewa kukidhi malengo ya kuwa na katiba mapema kabla ya kufi kia muda wa kuanza chaguzi za serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
.Hali hii ya kukwamisha zoezi itaweza kutufikisha kutenda dhambi ya kurefusha ratiba, kama walivyofanya Kenya ambapo waliongeza mwaka mzima mbele ya ratiba yao ya uchaguzi, jambo ambalo halina uhalali wa kikatiba wa kuwa na muhula wa miaka mitano ya uongozi zaidi ya utashi binafsi na uchu wa kuendelea kuwepo madarakani miongoni mwa sisi wabunge tuliopo sasa, tuhuma ambayo tutapaswa kuikiri kama ilivyo, guilty as charged.
  Juzi Rais Kikwete alikutana na viongozi wa vyama sita vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, Ikulu na kukubaliana mambo makuu mawili. La kwanza, vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, kuyawasilisha haraka serikalini ili kutafuta namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.
  La pili, vyama vya siasa nchini,kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya,viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato mabadiliko ya katiba ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali wa taifa.
  Katika makubaliano hayo, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini vitatu vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi viliwasilisha waraka wa ushirikiano wa vyama vya upinzani kwa Rais Kikwete.
  Waraka huo unamshauri Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kukataa kuukubali muswada huo, ambao vyama hivyo viliulalamikia kuwa una kasoro.Viongozi ambao alikutana nao kwa mazungumzo ni CCM, CHADEMA, CUF, NCCRMageuzi,TLP na UDP.
  Hata hivyo kumekuwepo na taarifa kuwa tayari Rais Kikwete amesaidia mswada huo tangu Oktoba 10, mwaka huu.Mwandishi wa makala haya ni Dkt. Hamisi Kigwangalla, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nzega na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI).

 

2 comments:

  1. Hongera kwa makala bora. Umekwenda shule wewe kweli. Tunasubiri kwa hamu mambo mapya ya upinzani ndani ya mchakato huo. Pia tunategemea kuwa sio kila jambo litaondolewa na wale waliopitisha mswaada wa awali.

    wanachi wafuatilie kwa makini na kujifunza kwa uangalifu nini kitakua haki yao mpya zaidi ya ile ya mwanzo.

    Isije kulinda walioko madarakani ama kuingiza wengine madarakani. Wasiruhusu kutumiwa kujenga umaarufu wa kundi lolote bali wajaribu kuvumbua mslahi na haki mpya itakayowawezeshesha kujiimarisha kiuchumi na kijamii

    ReplyDelete
    Replies
    1. Usimsifu KIGWANGALA, kumbuka wabunge wa upinzani walipotoka bungeni yeye na the infamous Komba,Nkamia,Kibajaj,walianza mipasho na matusi badala ya kujadili mswaada! Kama sio unafiki mawazo haya si angetoasiku hiyo. TUSIUTUKUZE UJINGA NA UNAFIKI

      Delete