Na Rachel Balama
Hospitali ya Kimataifa ya upasuaji wa moyo inatarajiwa kujengwa
nchini na Hospitali ya PARAS iliyopo nchini India
baada ya kuvutiwa na mazingira ya uwekezaji yaliyopo nchini Tanzania.
Hayo yalisemwa
na mbunge wa zamani wa Njombe kwa tiketi ya CCM, Yono Stanley Kevela, wakati
akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mara baada ya ziara yake ya mwezi
mmoja nchini India
kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wawekezaji kuja
nchini.
Kevela alisema
Watanzania wengi wanalazimika kwenda nchini India kutibiwa maradhi mbalimbali
kutokana na utaalamu huo kukosekana nchini, hivyo ujio wa hospitali hiyo
utakuwa fursa ya kipekee.
Alisema ujenzi
wa hospitali hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa Watanzania wa kipato cha chini
ambao hawana uwezo wa kusafiri kwenda nchini, India kwa matibabu hayo.
Alisema gharama za matibabu nchini India ni rahisi
ila kinachowakwamisha Watanzania wengi kwenda ni usafiri na gharama za kuishi
nchini humo.
Kevela ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya Yono Auction Mart, alimtaja Dkt. Kapil Gargi ambaye ni mratibu wa
kanda wa hospitali ya PARAS kwamba ndiye atakuwa mratibu wa mradi wa ujenzi wa
hospitali hiyo.
"Tuna tatizo la
watu kutokupima afya zao, mfano unaweza kumpeleka mgonjwa India kwa
matibabu lakini wewe unayemsindikiza mgonjwa ukipimwa unakutwa ndiye mgonjwa
zaidi ya yule uliyempeleka," alisema Kevela.
Aliongeza kuwa licha ya maji kuwa na umuhimu
mkubwa katika ujenzi wa mwili imara, lakini watu wengi hawana utamaduni wa
kunywa maji mengi hadi pale wanaposhauriwa na madaktari.
Kevela alisema amezungumza na Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi ambapo ameonyesha kufurahia mpango huo
na kuwataka Watanzania wengine kuiga mfano wa Kevela kuhamasisha wawekezaji
kuja hapa nchini.
Pia alisifu jitihada za Balozi wa Tanzania nchini India,
Injinia John Kijazi za kuhamasisha wawekezaji nchini India kuja kuwekeza hapa nchini na
kwamba hata PARAS imevutiwa kuja kuwekeza kutokana na jitihada za balozi huyo.
No comments:
Post a Comment