Na
Mwandishi Maalumu, OWM
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewahimiza viongozi wa
Kanisa la Moravian Jimbo la Ziwa Tanganyika kuwekeza zaidi kwa
vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.Alitoa wito huo jana wakati
akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Kigoma waliohudhuria sherehe za
Uzinduzi wa Jimbo la Ziwa Tanganyika Kanisa la Moravian Kigoma
. Waziri Mkuu ambaye alikuwa
mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, alimuomba Askofu Dkt. Isack Nicodemo wa Kanisa
la Moravian Tabora ambaye ndiye mlezi wa jimbo hilo
jipya, kuhakikisha kuwa anawapeleka vijana wengi wa Kanisa hilo kwenye Chuo cha Kilimo cha Mubondo
kilichopo wilayani Kasulu, Kigoma ambacho kinatoa mafunzo ya kilimo kwa vijana
katika ngazi za Astashahada na Stashahada ya Kilimo.
"Wakati nikiwa
vijijini, nimeona kuwa licha ya Mkoa wa Kigoma kuwa na ardhi nzuri na ya
kutosha, wananchi wengi wanalima bila ya kutumia kanuni bora za kilimo. Hivyo,
niliuelekeza uongozi wa chuo hicho kuweka kozi maalumu kwa watu wasiohitaji
cheti kwa ajili ya kuajiriwa, wapatiwe kozi maalumu kwa lengo la kuwawezesha
kutumia mafunzo hayo kubadili kilimo walichonacho na kukifanya kuwa na tija
zaidi.
"Nitoe
wito kwa Kanisa kuendeleza miradi hii ya kilimo kwa vijana kwa njia ya vikundi,
muwasaidie kwa kuwaelekeza ili vikundi hivi visajiliwe ili kuwawezesha vijana
hao kukopesheka na kupata misaada ya aina mbalimbali. Pia, muwawezeshe
kuzalisha kitaalamu, kuyaongezea thamani mazao yao kabla ya kuyauza, kupata nembo za ubora
kwa ajili ya bidhaa zao na kupata masoko ya uhakika," alisema.
Alisema,
kanisa na wakazi wa Kigoma wana fursa ya kukitumia Chuo cha Ufundi na Mafunzo
Stadi Nyamidoho kilichopo wilayani Kasulu kinachojengwa na Serikali kwa
kushirikiana na Shirika la World Vision ambacho lengo lake kuu
ni kutoa mafunzo ya kuongezea vijana wa mkoa huu stadi mbalimbali za kazi.
"Nilipata fursa ya kuweka jiwe la msingi
katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo Stadi Nyamidoho wilayani Kasulu ambacho
nimesema kipandishe hadhi na kuwa chuo cha wilaya hiyo. Nawasihi waumini wa
jimbo hili kuvitumia vyuo hivyo kikamilifu kwa kuwajengea stadi za kazi vijana
wetu ili wawe chachu ya mabadiliko katika vijiji vyao, mkoa huu na Taifa kwa
ujumla," alisisitiza.
Alitumia
fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa jimbo hilo
kwa juhudi zake za kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kuhamasisha jamii
kuwa na mazoea ya kupanda miti.Katika ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma,
Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI),
Hawa Ghasia, Waziri wa Kilimo na Chakula, Christopher Chiza, Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Maji, Dkt. Binilith
Mahenge pamoja na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
No comments:
Post a Comment