Na Eckland
Mwaffisi
Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa Tanzania haiwezi kuendelea kwa
mijadala isiyoisha na vikao vya kulipana posho bali kwa viongozi kufanya
maamuzi na kuyatekeleza haraka.Alisema Tanzania
inachelewa kupata maendeleo ya haraka kwa sababu kila mtu anayepewa kazi
anataka kuanza kujadili badala ya kuchukua maamuzi na kuyatekeleza.
Rais Kikwete
alimetoa tahadhari hiyo ya kuchelewesha maendeleo wakati akizindua Kambi ya
Vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani.Akizungumza na
wananchi kabla ya kuzindua kambi hiyo na kukagua shughuli zinazofanywa na
vijana 50 kutoka vijiji vya Wilaya ya Rufiji ambao wanajifunza mbinu na maarifa
ya kilimo bora katika kambi hiyo, alitaka kujua kama
kampuni mbili zilizoomba ardhi ya kulima kisasa katika Bonde la Mto Rufiji,
zimepewa ardhi ya kuanza kulima.
Awali katika
maelezo yaliyosomwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la
Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja, yaliashiria kuonesha kampuni hizo
Frontline Development Partners na Lukurilo Holdings Company Limited, yalipewa
ardhi na Mamlaka hiyo kama yalivyokuwa yameomba.
Pamoja na maelezo hayo, Rais Kikwete alipotaka kujua kampuni hizo
zilipewa ardhi kiasi gani Bw. Masanja alisema Frontline Development Partners
walioomba hekta 20,000 lakini walikuwa hawajapewa hata moja na Lukurilo
Holdings walioomba hekta 12,000 na kupewa 4,000 tu.
Rais Kikwete alishangazwa na hali hiyo na kusema; "Kwa miaka minne
sasa, tunazungumza jambo hili bila kufikia uamuzi wake, tumewahi kujadili suala
hili pale Ikulu, Dar es Salaam
na kukubaliana, nini kimetokea.
"Tulikubaliana kutekeleza jambo hilo
sasa tunaendelea kujadili nini, nchi yetu itachelewa sana kupata maendeleo kwa sababu kila mtu
anayepewa kazi anataka kuanza kujadili," alisema.
Aliongeza kuwa, Tanzania
haiwezi kuendelea kwa mijadala na vikao vya kulipana posho visivyoisha kwani
Frontline Company imeanza kuomba ardhi ya kulima miaka mitano iliyopita.
Aliwataka viongozi wote wanaohusika na suala hilo kukutana wiki ijayo na kusisitiza kuwa,
nchi inakwamishwa na watu wa namna hiyo.
Mapema Rais Kikwete amewaambia viongozi wa kambi hiyo ambayo inamilikiwa
na RUBADA kuwa, kazi ya kambi hiyo iwe kuandaa vijana wa kujiajiri kwa kilimo
cha kisasa si kuandaa watu wa kutafuta kazi ya kuajiriwa katika kilimo.
"Tunaandaa wakulima wazuri, vijana
si kuandaa kundi la watu wa kutafuta ajira ya kilimo, hatuwezi kuwa na kambi ya
namna hii ikiandaa kundi la watu wa kutafuta ajira, kijijini utaajiriwa na nani
kama siyo kushiriki kilimo," alihoji Rais
Kikwete.
Alisema amefurahishwa na uamuzi wa kuandaa vijana hao ili waweze
kushiriki katika kilimo kwa sababu mageuzi ya kilimo yataletwa na vijana. Rais
Kikwete alizindua mradi mkubwa wa maji Mjini Kibiti na kukabidhiwa boti ambazo
zitafanya shughuli za kubeba wagonjwa katika maeneo ya Nyamisati na visiwa vya
jirani.
No comments:
Post a Comment