Na Speciroza Joseph
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya
Vodacom, Yanga jana wameibamiza Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika mechi ya ligi
hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.Mtibwa ilianza kwa kasi
ambapo dakika ya nne mshambuliaji wake Vicent Barnabas aliachia shuti kali
lililookolewa na kipa wa Yanga, Ally Mustafa 'Bathez'.
Yanga ilianza kupata bao
dakika ya sita kupitia kwa Mrisho Ngassa, baada ya kuwatoka mabeki wa Mtibwa na
kuachia shuti lililompita kipa, Hussein Shariff.Dakika ya kumi Yanga
ilifanya shambulizi langoni mwa Mtibwa ambapo, Simon Msuva aliachia shuti kali
lililotoka nje ya lango.
Mussa Hassan 'Mgosi' wa Mtibwa
Sugar dakika ya 15 alikosa bao la wazi akiwa katika nafasi nzuri, lakini
akajibabatiza na mpira kuwahiwa na mabeki wa Yanga.Didier Kavumbagu wa Yanga dakika ya 18 aliachia shuti kali langoni mwa
Mtibwa ambapo mpira uligonga mwamba na kuokolewa na kipa wa Mtibwa.
Yanga ilipata bao la pili dakika
ya 23 kupitia kwa Kavumbagu baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Msuva.Dakika ya 44 Mgosi aliikosesha Mtibwa bao, baada ya kubaki na kipa wa
Yanga, lakini shuti lake likadakwa na kipa huyo, huku Kavumbagu naye akikosa
bao katika dakika hiyo kutokana na shuti lake kutoka
nje kidogo ya lango la Mtibwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuingia kwa nguvu ambapo Hamis
Kiiza, aliikosesha timu bao la wazi baada ya kushindwa kumalizia krosi nzuri
iliyochongwa na Nizar Khalfan.Mtibwa ilizinduka dakika ya 70, baada ya Shaban Kisiga kuachia shuti
kali langoni mwa Yanga ambapo mabeki waliokoa hatari hiyo.Dakika ya 72 Mtibwa
ilifanya shambulizi la kushtukiza lakini shuti la mbali la Juma Luzio,
liliokolewa na kipa Bathez.
Kisiga alijaribu
tena kuachia shuti kali lililookolewa na kipa wa Yanga na mpira kutoka nje ya
lango. Masoud Mohamed 'Chile'
aliikosesha Mtibwa bao dakika ya 84 akiwa yeye na lango lakini shuti lake likapaa
nje ya lango.
No comments:
Post a Comment