Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
imemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya
ukaguzi wa mahesabu haraka iwezekanavyo katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi ili kuondoa sintofahamu ya mahesabu yake, anaripoti
Anneth Kagenda.
Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Bw. Gaudence Kayombo, alipokutana na watendaji wa Wizara hiyo
akiwemo Katibu Mkuu, Profesa Sifuni Mchome.“Hatusemi fedha imeliwa hapana ila
tumeagiza ukaguzi ufanyike mara moja ili kubaini ukweli wa hesabu zenu...pamoja
na kwamba majibu ya Katibu Mkuu yanaridhisha, lengo letu ni kupata majibu ya
kueleweka,” alisema Bw. Kayombo na kuongeza;
“Mfano Wizara imetoa milioni kadhaa kwenda Mkwawa au katika vyuo na
taasisi za elimu... tunachotaka tukiangalia taarifa za huko tukute zinafanana
zisikinzane lakini tunaamini baada ya CAG kufanya ukaguzi wake tutabaini tatizo
liko wapi,” alisema.
Aliongeza kuwa, uhamishwaji fedha kwenda kwenye taasisi bado
haujaeleweka na unakinzana na kutoa mfano kuwa, Wizara hiyo imepeleka fedha
ADEM Bagamoyo ambazo zinaonesha sh. milioni moja lakini taasisi husika itasema
ilipokea zaidi au pungufu.
Bw. Kayombo alisema umefika wakati wa watendaji katika wizara hiyo,
kuhakikisha wanaisaidia Wizara iweze kufanya shughuli zake vizuri badala yake
wamekuwa wakimwangusha Katibu Mkuu ambaye anaonekana kuwa na majibu ya uhakika
pale anapotakiwa kufanya hivyo.
Alisema watendaji hao, mwaka 2012 walipewa mambo matano ya kufanya
lakini cha kushangaza wamefanya jambo moja ambalo ni kutembelea Shule ya
Sekondari ya Miono, iliyoko Mjini Bagamoyo, mkoani Pwani na taarifa imeonesha
shule hiyo inahitaji uzio.
“Shule hii iko karibu na Mbuga hivyo tulishauri iwekwe uzio, hilo tu ndiyo walilofanya lakini tuliwaagiza waangalie ada
za wanafunzi wa vyuo vya juu jambo hilo
bado halijafanyika,” alisema.Aliongeza kuwa, Bodi ya Mikopo pia ilitakiwa kutoa
maelezo ya utoaji mikopo kwa wanafunzi, kuangalia uwezekano wa kujiendesha
yenyewe badala ya kuitegemea Serikali badala yake bodi hiyo ilikwenda na
mkakati wake.
Prof. Mchome, alipoulizwa juu ya mkanganyiko wa fedha hizo alisema;
“Nadhani hili ngoja likafanyiwe kazi lakini ninachojua hakuna fedha iliyoliwa,”
alisema. Akizungumzia suala la ukusanyaji mikopo, alikiri bado jitihada kubwa
zinahitajika katika ukusanyaji huo.
No comments:
Post a Comment