23 October 2013

KESI YA PINDA YAKWAMA



   Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kikatiba aliyofunguliwa Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), anaripoti Rehema Mohamed. Hali hiyo ilitokana na kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Naibu AG, George Mwasaju kutokuwepo mahakamani hapo
.  Kesi hiyo ipo mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na jaji Fakhi Jundu, ambapo jana ililetwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, lakini kabla ya usikilizwaji huo, Wakili Mkuu wa Serikali, Gabliel Malata aliiarifu mahakama kuwa wana ombi.
Malata alisema Naibu AG alipata taarifa za dharura juu ya uwepo wa mkutano wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaohusu masuala ya sheria ulioanza jana hadi Oktoba 28 mwaka huu mkoani Arusha, katika Makao Makuu ya EAC.
Alidai wajumbe wa mkutano huo ni Wanasheria wakuu na Manaibu wake wa nchi tano za jumuiya hiyo na hakukuwa na namna ya yeye kutohudhuria mkutano huo ambapo kukosekana kwake kungesababisha mkutano huo kutofanyika.
Aliongeza kuwa, tayari Naibu AG lishaandika barua ya kuitaarifu mahakama hiyo na upande wa waleta madai kuhusu mkutano huo.“Waheshimiwa Majaji, Naibu AG ndiye aliyekuwa akiongoza jopo la mawakili wa Serikali katika shauri hili, kutokana na sababu niliyoainisha hapo awali, tunaomba ahirisho hadi baada ya mkutano huu kuisha ili na yeye aweze kuhudhuria kesi na kusikiliza hoja za upande wa pili,” alidai Malata.
Kutokana na asili ya shauri hili, anaomba ombi hilo likubaliwe kutokana na sababu nilizotoa,” aliongeza. Akizungumza kwa niaba ya upande wa waleta madai, wakili Mapare Mpoki alikubaliana na ombi la upande wa Serikali hivyo Majaji wa kesi hiyo waliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8-11, mwaka huu.
 Pinda na AG walifunguliwa kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 na wanaharakati wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), pamoja na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakidai Bw. Pinda amevunja katiba ya nchi.
 Hatua hiyo ilitokana na kauli ya Bw. Pinda aliyoitoa bungeni, katika mkutano wa 11 wa Bunge, akiwapa maelekezo na amri watekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.Kauli hiyo ilitolewa bungeni Mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo, Juni 20 mwaka huu, wakati Bw. Pinda akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, aliyetaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.
Bw. Pinda alisema; “Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... eeh, hamna namna nyingine, eeh maana lazima tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh maana tumechoka,” inasomeka hati ya madai ikimnukuu Bw. Pinda.
Katika kesi hiyo, walalamikaji wanadai kauli hiyo ni kinyume cha katiba kwa kuwa inakiuka Ibara za 12(2) 13(1), 13(3), 13(6)(a-e), hivyo wanaiomba mahakama, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha katiba na imwamuru Bw. Pinda aifute hadharani.Wanadai kauli na amri kama hizo, zinapotolewa na kiongozi mwenye hadhi kama ya mdaiwa, zinachukuliwa kama sheria inayopaswa kutekelezwa na wakala.

2 comments:

  1. Hawa wanasheria hawana kazi za kuwasaidia wananchi, kuna wananchi wanashida sana na wanahitaji sana msaada wa kisheria , waende huko

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wao wanaona sifa kupandana na jambo lisilo na tija. Wakamsaidie kiongozi wa chadema aliyepigwa na wenzake huko Arusha!
      Eti wanakosoa wenzao wao wakikosolewa wanakua wakali zaidi ya simba. Ngonja waingie madarakani ndyo mtajua mbivu na mbichi!

      Delete