07 October 2013

UTAPELI UBUNGO WARUDI 'KIAINA', KWA ABIRIA



 Na Mwandishi Wetu
  Siku chache baada ya Gazeti la Majira kuandika habari zilizohusiana na utapeli waliokuwa wakifanyiwa abiria katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT), hali si shwari tena ndani ya kituo hicho
.  Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, lilifanya kazi kubwa ya kuusambaratisha mtandao huo baada ya habari hiyo kutoka gazetini na kurudisha hali ya usalama kituoni hapo. Mwenyekiti wa Kata ya Ubungo Magorofani, Aman Sizya, alisema hivi sasa ndani ya kituo hicho kumeibuka Vikundi vya Ulinzi Shirikishi ambavyo ofisi yake haivitambui.
  Alisema vikundi hivyo ambavyo vinadaiwa kuwekwa na mawakala wa mabasi, vinafanya kazi ya kunyanyasa abiria na wengine kuwaibia mizigo yao hivyo jitihada za polisi kuvunja mtandao wa awali, hazijazaa matunda.
  "Baadhi ya walinzi shirikishi wanaotoka katika vikundi hivi, wametengeneza vitambulisho ambavyo vina namba yangu ya simu lakini havina muhuri wa Manispaa ya Kinondoni kama ilivyo kwa walinzi halali ambao idadi yao ni 12," alisema.
  Alisema kama uongozi wa kituo hicho na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni hawatachukua hatua stahiki dhidi ya vikundi hivyo, vinaweza kuharibu sifa ya kituo kwa abiria na Taifa."Ubungo kunafuka moshi, kuna siku litatokea tatizo kubwa ambalo chanzo chake ni hawa walinzi shirikishi ambao sisi kama Serikali ya Kata na Ofisi ya Mtendaji Ubungo hatuwatambui.
  "Mambo yanayofanyika katika kituo hiki kwa sasa yanatisha, abiria wananyanyaswa na kuibiwa mali zao, tulizungumza suala hili lakini bado linaendelea," alisema Sizya.Alisema ofisi hizo za Serikali zinawatambua walinzi shirikishi waliopangiwa kufanya kazi ndani ya kituo hicho lakini inashangaza kila wanapoingia ndani, hutimuliwa na vikundi hivyo.
  "Kituo cha Ubungo ni sawa na shamba la bibi kwa sababu abiria wengi wanaotoka na kwenda mikoa mbalimbali wanatumia kituo hiki, tatizo hili linachangiwa na mawakala wa mabasi ambao niliwaambia waniletee barua za maeneo ambayo walinzi wao wanatoka lakini hawakufanya hivyo," alisema.
  Sizya alisema ,awali aliwaambia walinzi hao (wasiotambulika),wajisalimishe lakini waligoma badala yake wanatumia ubabe kufanya kazi hiyo wakati hawatambuliki na wengi wao hawaishi Ubungo.Awali Sizya alishiriki uzinduzi wa uhakiki kwa madereva wa pikipiki zinazobeba abiria 'bodaboda' na bajaji uliofanywa na Shirika la Elimu ya Usafiri (SEUTA), chini ya Mwenyekiti wake Hussen Hassan.
  Katika uzinduzi huo, ilibainika kuna vitendo vya ukatili na unyanyasaji unaofanyika Ubungo hivi ipo siku kunaweza kutokea tatizo kubwa na la hatari kwa wananchi ambao wanafanya shughuli zao ndani ya kituo hicho.

No comments:

Post a Comment