Na Anneth Kagenda
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imesema katika utafiti
wake kwenye halmashauri mbalimbali nchini, imebaini kuna mchezo mchafu
unaofanywa ambapo vitendo vya ufisadi mkubwa vinaanzia Hazina.
Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Rajabu Mohamed Mbaruku aliyasema hayo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam
kwenye ukumbi mdogo wa Bunge ambapo kamati za Bunge zinaendelea.
Alisema, pia
vitendo vya ufisadi vinafanywa na watendaji katika Ofisi za mikoa.
Alisema, kabla
ya kamati hizo kuanza, kamati yake ilizunguka katika halmashauri na mikoa
mbalimbali ukiwamo Mkoa wa Lindi, Tabora, Morogoro ambapo ilibaini ufisadi huo
unafanyika na wanaoufanya ni watendaji ofisi za mikoa na Hazina.
"Kamati
yangu ilianza ziara tangu Oktoba Mosi, lakini pia tulibaini ufisadi huo
unaofanywa na watendaji wa mikoa na Hazina ambapo wakati mwingine hazina inadai
kuwa, fedha zilishapelekwa na ukiziuliza halmashauri zinadai hazijapata fedha
hiyo,"alisema Mbaruku.
"Fedha za
halmashauri toka hazina haziwafikii, taarifa zinasema zimeenda, lakini ukiuliza
wahusika wanadai hazijafika pia tumebaini matatizo mengi ya halmashauri
yanafanana, kwani utakuta wameainisha fedha walizopokea, walizotumia, lakini
ukiangalia mchanganuo wa matumizi haueleweki,"
"Sasa
hatujui kama wanataka kuiongopea kamati au
fedha zile wamezichakachua wenyewe... Watendaji katika uvujaji wa fedha za
halmashauri kumbukumbu zimekuwa hazioani, mfano utakuta anasema zilizopelekwa
ni sh.milioni kadhaa, lakini ukiangalia uhalisia utakuta
haviendani,"alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema, katika halmashauri mbili
walizokutana nazo jana halmashauri ya Mbulu fedha za Mradi wa Umeme Vijijini
(REA) sh. milioni 170 zilipelekwa ambapo sh. milioni 120 zinaonekana zilitumika
ila mchanganuo hauoneshi zilitumika vipi na kusema kuwa, hivyo wameidanganya
kamati yake na fedha zimeliwa.
Mwenyekiti huyo pia alisema, wamebaini fedha
asilimia 10 za Mfuko wa Wanawake na Vijana ambazo wanatakiwa kuwa wakikopa na
kurejesha ambapo halmashauri hutakiwa kuzitoa nazo zimekuwa zikiliwa.
"Katika mfuko huo wanawake wana asilimia
tano na vijana asilimia tano, lakini halmashauri hizo hazipeleki fedha hizo
badala yake wanazichakachua pia Halmashauri ya Mbulu tangu kuanzishwa kwa
sheria hiyo, miaka mitano iliyopita haijawai kupeleka hata senti tano,"
alisema.
Alisema, kwa mantiki
hiyo Mbulu imeamriwa kulipa fedha hiyo mara moja na kusema kuwa katika mfuko
huo fedha za serikali zimekuwa zikipelekwa ila halmashauri ndio vikwazo.
Aidha, alisema baada
ya serikali kuondoa kodi kuna asilimia 20 ambayo inatakiwa kwenda vijijini
ambapo ilitaka halmashauri kuwa zikipeleka asilimia hiyo, lakini cha kushangaza
fedha hizo haziendi ambapo alisema kuwa hali hiyo inaonesha kuwa halmashauri
zimeonekana kuwa kidonda ndugu cha kuua maendeleo ya nchi.
Alisema, katika wiki mbili watakazokuwa kwenye kamati
wanatarajia kuzihoji halmashauri 16 na kwamba jana walikuwa na halmashauri ya
Babati na Mbulu ambapo pia wamebaini madudu Mbulu.
Thanks great blog
ReplyDelete