Penina Malundo na Revina John
Madereva wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani katika Kituo cha
Ubungo, jijini Dar es Salaam jana yamegoma kwa
takriban saa sita wakishinikiza Serikali kutowatoza faini ya asilimia tano ya
uzito unaozidi kwenye magari yao
yanapopimwa kwenye mizani.
Mgomo huo
ulioanza saa 12 asubuhi ulisababisha adha kubwa kwa abiria, huku madereva hao
wakiwa wameshikilia msimamo wa kutoanza safari pasipo mwafaka kupatikana kati
ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania
(TABOA) na Serikali.
Dai jingine ni
kuitaka Serikali kusitisha utaratibu wa kupima mabasi kwa madai kwamba mizani
hiyo imekuwa ikitofautiana vipimo kutoka kituo kimoja hadi kingine.
Abiria
waliokuwa wasafiri na mabasi hayo walilazimika kusubiri hadi saa sita mchana
ambapo magari ya kwanza yalianza kuondoka Ubungo badala ya saa 12 asubuhi baada
ya Serikali kuingilia kati.
Mgomo wa madereva hao wa mabasi ulionekana
kuzidiwa nguvu kutokana na wenye kampuni za magari hayo kukatisha tiketi kwa
abiria wakati wakijua kwamba hawatawasafirisha.
Abiria wengi walihoji sababu za wenye mabasi
hayo kuchukua fedha zao za tiketi wakati wakijua hakutakuwa na safari.Usafiri
wa mabasi kutoka Ubungo ulianza saa sita mchana baada ya kufikia mwafaka wa
awali kati ya viongozi wa SUMATRA, Polisi na
TABOA.
Wenye mabasi hayo waliamua kuanza safari jana
baada ya Serikali kukubaliana nao kuwa siku ya jana mabasi hayo hayatapimwa
uzito kwenye mizani.Hata hivyo, waliendelea kusisitiza kuwa leo hawatasafirisha
abiria wala kukatisha tiketi iwapo mwafaka hautakuwa umepatikana baina ya
Serikali na TABOA.
Akizungumza na gazeti hili Mjumbe wa Kamati
Kuu ya TABOA, Rajabu Kasimu, alisema madai yao ni muda mrefu, lakini kutokana na
kutopatiwa ufumbuzi ndiyo maana wameamua kugoma.
“Tulitoa tangazo la mgomo leo (jana) kwa
takriban siku nne ziliziopita, lakini tulikutana na Waziri Mkuu (Mizengo Pinda)
akatuambia tusitishe mgomo wakati ufumbuzi ukitafutwa, lakini hadi juzi
hatukuona utekelezaji wowote ndiyo maana tumefikia hatua hii," alisema Kasimu.
Alisema kamati yao
ilikutana na baadhi ya viongozi wa SUMATRA
pamoja na Jeshi la Polisi ili kutafuta ufumbuzi, ndio maana wameamua kuanza
safari kwa jana kwa sharti kuwa hakuna mabasi hayo kupimwa.
Kwa Upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohammed Mpinga, aliagiza mabasi yaliyogoma kuanza safari mara moja
na wale watakaokaidi watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni
zao.
“Nimesema kuanzia
sasa mabasi yaondoke na yale yatakayokaidi agizo langu tumekubaliana na wenzetu
wa SUMATRA kuwachukulia hatua za kisheria
ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni,” alisema Mpinga.
Ofisa wa Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA)
Gervas Rutaguzinda, alisema amesikitishwa na kitendo cha mabasi hayo kugoma na
kugeuza abiria kuwa mateka. Meneja Leseni wa SUMATRA, Leo Ngowi, aliwataka
madereva kusitisha mgomo huo na kuendelea kutoa huduma kwa abiria kama awali
wakati suala hilo
likitafutiwa ufumbuzi.
Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Wizara
ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema sheria bado iko pale pale haijabadilishwa. Alisema
chanzo cha malalamiko hayo ni kufukuzwa karibu asilimia 85 ya wafanyakazi
kwenye mizani ambao walikuwa wamezoeana na wafanyabiashara. “Sasa hivi
wafanyabiashara wanapata shida kuzoeana na wafanyakazi wapya kwenye mizani ndiyo
maana wanalalamika,” alisema
No comments:
Post a Comment