Na Godfrey Ismaely
Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) kimemtaka
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara kuondoa
adhabu kwa magazeti yaliyofungiwa yakiwemo Mwananchi, Mtanzania na Mwanahalisi
bila masharti
. Wamiliki wa
vyombo vya habari nchini walikutana na kujadili suala la Serikali kutoa adhabu
za kufungiwa magazeti ambazo zinatolewa mara kwa mara kama
yalivyofungiwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa vipindi tofauti kuanzia
Septemba 27, mwaka huu.
Kwa mujibu wa
taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa MOAT, Henry
Muhanika ilibainisha kuwa, kikao cha MOAT jana kilikubaliana mambo makuu manne
ya msingi."Tuhuma zilizotolewa dhidi ya magazeti yaliyofungiwa zilikuwa za
jumla na hivyo hazikukidhi haja ya kuhalalisha adhabu iliyotolewa.
"Pili kitendo cha kufungiwa magazeti
kinaingilia haki ya wananchi kupata habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari
kupata ajira," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa,
jambo la tatu ambalo wamiliki hao walikubaliana ni kwamba uamuzi wa kuyafungia
magazeti unafanywa bila kufuata taratibu na kanuni zinazotakiwa ikiwemo haki ya
watuhumiwa kuitwa na kusikilizwa.
Jambo la nne taarifa hiyo ilibainisha kuwa,
kitendo cha kufungiwa magazeti kinapunguza hadhi ya Serikali na kinamchafua
rais ndani na nje ya nchi. Aidha, wamiliki wa vyombo vya habari waliishauri
Serikali iachane na utaratibu wa kufungia magazeti bali pale inapoona yametokea
matatizo itumie mazungumzo na maelewano au ipeleke kesi mahakamani badala ya
kuwa mlalamikaji na hakimu.
No comments:
Post a Comment