- ASEMA MEZA YA MAZUNGUMZO ITATOA MWAFAKA
- ADAI KUSAINI MSWADA NI KUIUNGA MKONO CCM
Rachel
Balama na Grace Ndossa
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Bw. Tundu Lissu, amesema kama Rais Jakaya Kikwete ana dhamira ya kusikiliza kilio
chao kwa njia ya mazungumzo, asisaini Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba 2013 ambao umepitishwa na Bunge, Mjini Dodoma, hivi
karibuni
. Bw. Lissu
aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu
ya mgogoro uliojitokeza bungeni kuhusu mswada huo na suala zima la mchakato wa
Katiba Mpya.Alisema kama
Rais Kikwete amedhamiria kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani akiamini
kilio chao kinazungumzika kwa njia ya mazungumzo ili kufikia mwafaka, asisaini
mswada huo.
"Kwa
mujibu wa Katiba, Rais ana mamlaka ya kukataa mambo yasiyo na masilahi kwa
wananchi na Taifa yanayopitishwa bungeni, ombi letu asisaini mswada huu na kama atafanya hivyo, atakuwa anawaunga mkono wabunge wa
chama tawala CCM," alisema.Aliongeza
kuwa, mswada huo una kasoro nyingi hivyo ni vyema ukafanyiwa marekebisho kabla
hajausaini ili Watanzania waweze kupata Katiba Mpya waitakayo si vinginevyo.
Bw. Lissu
alisema ni vyema mazungumzo hayo yakafanyika haraka kwani mchakato wa Katiba
ukivurugwa, nchi inaweza kuingia katika machafuko yanayoweza kuzuilika."CCM inataka kuingilia mchakato huo ili
kulazimisha mambo ya Muungano ndio maana wanafanya jitihada mbalimbali ili
kuuvuruga mchakato huu," alisema Bw. Lissu.
Akizungumza katika hotuba yake ya kila mwezi,
Rais Kikwete alisema madai ya upinzani yanazungumzika, mengine yangeweza
kukubalika kama wabunge wake wangekuwepo
bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha miswada.Alisema kutokuwepo kwao bungeni, hapakuwa na
mtu wa kuwasemea ambapo baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya
Bunge ni jambo lisilowezekana.
"Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo
hujadiliwa na kuamuliwa bungeni si vinginevyo, kuandamana nchi nzima au
kuchukua hatua za kutotii sheria kama
Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko
ambayo wanayataka katika sheria hii, naamini na wao wanautambua ukweli
huo," alisema Rais Kikwete katika hotuba hiyo.
Aliwataka viongozi (Wenyeviti) wa vyama vya
CHADEMA, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), waongozwe na hekima kutumia
utaratibu uliotumika mwaka 2012 baada ya kutokea mazingira kama
hayo, pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine,
kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi.
Alisema
baada ya kuridhiana, hatua zipasazo za kisheria na kanuni, zilichukuliwa na
kumaliza mzozo hivyo kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huo
zaidi ya kuliingiza Taifa katika matatizo yasiyo ya lazima. Rais Kikwete
alisema iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule, inaweza kufanya hivyo hata
sasa
No comments:
Post a Comment