Na Mwandishi Wetu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), limetangaza viingilio vya mechi ya Simba na Yanga Ligi Kuu ya Vodacom
itakayopigwa Jumapili Uwanja wa Taifa ambapo cha chini kitakuwa sh. 5,000.Kiingilio
cha sh. 5,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa
Habari wa TFF, Boniface Wambura, kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio
ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C sh. 15,000,
VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tiketi moja itapatikana
kwa sh. 30,000.
“Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja
kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni katika vituo mbalimbali.“Vituo
hivyo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers
ulioko mtaa wa Ohio/ Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live
Mbagala, Uwanja wa Uhuru na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani,” alisema Wambura.
Wambura alisema mechi hiyo namba 63 itachezeshwa na Israel Nkongo kutoka Dar es
Salaam, ambapo atasaidiwa na Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam pia na Ferdinand Chacha wa
Bukoba. Mwamuzi wa akiba ni Oden Mbaga wa Dar
es Salaam.
Alisema Kamishna wa mechi hiyo atakuwa, John Kiteve kutoka Iringa wakati
mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Stanley Lugenge wa Njombe.
Wakati huo huo, Wambura alisema mechi tatu za Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) katika kundi A na C, zimesogezwa mbele kutokana na viwanja vya Kambarage,
Shinyanga na Nangwanda Sijaona, Mtwara kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
Alisema katika kundi A, mechi kati ya Ndanda na Transit Camp iliyokuwa
ichezwe Oktoba 19 mwaka huu sasa itafanyika Oktoba 21, mwaka huu kwenye Uwanja
wa Nangwanda Sijaona.
Ofisa huyo alisema Stand United na JKT Kanembwa zilizokuwa zicheze
Oktoba 19 mwaka huu, sasa mechi hiyo ya kundi C itafanyika Novemba 2, mwaka huu
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo mechi ya Mwadui na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo
Oktoba 26, mwaka huu imesogezwa hadi Novemba 3, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment