Na Lilian Justice, Morogoro
WAKAZI wa
kata tatu za Manispaa ya Morogoro wameiomba Serikali kupitia baraza la katiba
kuhakikisha marekebisho ya rasimu ya Katiba Mpya yanafafanua kwa kina masuala
ya kijamii ikiwemo kipengele cha afya, elimu na maji kufuatia vipengele vingi
kukosa ufafanuzi.
Wakazi hao walisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye
tamasha la sanaa ya uhamasishaji wananchi juu ya uchangiaji maboresho ya rasimu
ya Katiba Mpya lililoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Mapinduzi
Forum kwa kushirikiana na Shirika la Mkitunda baada ya kupewa baraka na Tume ya
baraza la katiba kupitia ufadhili wa The Foundation For Civil Society na
kufanyika katika kata tatu za Manispaa ya Morogoro ambazo ni Kihonda, Mazimbu
na Mafisa.
Maimuna Mabeja ni mmoja kati ya wananchi waliopata nafasi ya kushiriki
matamasha hayo na kutoa maoni yao ambapo aliomba baraza la katiba kuhakikisha
linatoa kipaumbele katika masuala ya jamii ikiwemo afya, elimu na maji kwa
kutoa ufafanuzi wa kina ili kuifanya jamii kujua umuhimu wao katika masuala
hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la mapinduzi Forum ambaye pia ni
Msimamizi wa mradi huo, Mkosasura Waziri alisema kuwa katika kuhakikisha
wananchi wanapata nafasi ya kuchangia maboresho ya rasimu ya Katiba Mpya
Mapinduzi imeamua kufanya sanaa shirikishi katika kata hizo kwa kufanya
maigizo, ngoma na kuibua mada ambazo wananchi wameweza kuchangia ili kuboresha
rasimu ya Katiba Mpya.
Waziri alisema kuwa mpaka sasa tayari wameshagawa rasimu za katiba 140
kwa wananchi wa kata hizo ambao wameshazipitia na kutoa maoni yao ambapo
wanatarajia kugawa rasimu za katiba 130 kwa wananchi watakaochaguliwa kushiriki
katika mdahalo waliouandaa utakaofanyika Agosti 26 na 27 mwaka huu ili wananchi
waweze kutoa maoni yao katika maboresho hayo.
Hata hivyo kwa
upande wa Ofisa Tawala wa shirika hilo, Zainabu Mkali alisema kuwa uhamasishaji
huo utasaidia wananchi hasa wale waliokosa nafasi ya kuchangia maoni ya katiba
mpya kuweza kutoa maoni yao katika maboresho ya rasimu ya katiba mpya kupitia
sanaa wanayoitoa.
No comments:
Post a Comment