27 August 2013

CHADEMA YAMJIBU DADA YAKE MBOWE



Na Goodluck Hongo
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakishangazwi na Grace Mbowe, ambaye ni dada wa Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe, kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani si jambo la kushangaza na chama hicho si cha kifamilia.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana ofisa habari wa chama hicho,Tumaini Makene alisema CHADEMA haioni ajabu kuhamia katika chama hicho na hakina pingamizi lolote.
"CHADEMA haioni kasoro na isitoshe kuwa chama hiki si cha familia wala kikabila kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiri," alisema.
Alisema masuala ya kisiasa yasiingizwe katika familia kwani wapo wanasiasa wengine ambao watoto wao ama ndugu zao wamejiunga na CHADEMA kutoka CCM na hakuna jambo baya lililofanyika juu yao.
Alisema kwa suala hilo si la kujadiliwa kwani ni suala la kisiasa ambalo halitakiwi kuhusishwa na masuala ya kiuchumi hivyo ni vyema Watanzania wakaelewa hilo.
"Ni lazima hata hao CCM wajiulize kuwa mtoto wa mwasisi wa chama na Taifa hili yuko chama gani? pia Mtoto wa Stephen Mashishanga yuko chama gani na hao ni wachache tu kwani wapo wengi lakini kuna kitu kilichotokea wala kuharibika nashughuli zinaendelea kama kawaida tu na kuhama kwake hakutaathiri chochote," alisema Makene.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa dada wa mwenyekiti wa chama hicho Grace Mbowe amejiunga na CCM na kukabidhi kadi yake kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Bw.Hassan Mtenga.
Bi. Grace alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa uamuzi wake wa kuwepo CHADEMA haukuwa uamuzi wa kifamilia hivyo hakuna wa kumuuliza kwanini anajiengua CHADEMA kwani huo ni utashi wake tu.

No comments:

Post a Comment