20 August 2013

WANANCHI WALALAMIKIA KUPUNJWA FIDIA



 Na Said Njuki, Kondoa
WA K AT I w a n a n c h i wa l i o j e n g a kwe n y e hifadhi ya barabara ya Mayamaya-Dodoma hadi Bonga mkoani Manyara wakilipwa fidia kupisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami baadhi ya wananchi hao wameishutumu Serikali kwa kuwalipa fidia kidogo.

Wananchi hao wa vijiji mbalimbali wakizungumza na waandishi wa habari juzi wamedai mbali na fidia hiyo ndogo, pia walitakiwa kuchukua hundi zao ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kondoa, kazi iliyochukua siku mbili na kuwagharimu fedha zaidi ya malipo waliyolipwa.
"Ni kweli tunahitaji maendeleo kwa faida yetu, lakini hatukutendewa haki, leo tunauza mazao kidogo tuliyopata shambani kwa ajili ya kupata nauli ya kufuatilia hundi, mara unakuta hundi yako ni shilingi 13,000/- na hapohapo unaambiwa ufungue akaunti, wengine majina yao hayaonekani kabisa, na unaambiwa uendelee kulalamika kwa barua zetu tumkabidhi mtendaji wa kijiji hii fidia haijaja kwa walengwa kabisa," alisema John Barnaba kwa Kijiji cha Masawi Kondoa.
"Wakati wa tathmini kulikuwa na matatizo ndio maana kulikuwa na matatizo zaidi, kwani baadhi ya viongozi walikuwa wanadai chochote ili kuandikiwa fidia, tena yule mama alikuwa hataki kuhojiwa kabisa sasa leo baadhi ya majina hayajaonekana kabisa, hata jina langu halipo naamini ni kwa sababu sikutoa chochote," alisema mmoja wa wananchi hao ambaye hakutaka jina lake kuwekwa bayana.
"Kwa nini majina mengine hayapo na wakati majina hayo yalikuwepo, kwa nini malipo yafanyike wilayani badala ya ofisi za kijiji na badala yake wananchi wanatumia fedha nyingi tofauti na malipo yao?" alihoji Mzee Delo wa Kijiji cha Masawi.
Pia wananchi hao wamedai kuwa tayari wamepewa notisi ya mita 30 ya miezi mitatu, wakati malipo yaliyofanyika ni ya fidia ya mita 22.5 jambo linalowapa wasiwasi mwingine kwa kuingia katika mgogoro usiokuwa wa lazima.
Serikali za vijiji vya Masawi, Bereko na Bukulu zimekiri kupokea malalamiko hayo na kwamba wanafanya taratibu za kuwakilisha malalamiko hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa kama walivyoelekezwa na mamlaka husika.
Kwa mujibu wa nakala ya notisi kwa wananchi hao toka Wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, imeeleza kuwa tayari mali zilizo ndani ya hifadhi ya barabara mita 30 kila upande kwenye barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 188.15 zimeshatathminiwa na kulipwa fidia stahiki, hivyo wanatakiwa kuondoa mali zao kwenye eneo hilo ndani ya siku 90 kupisha ujenzi wa barabara hiyo bila taarifa yoyote.
"Ili kuwezesha ujenzi wa barabara kuanza, unatakiwa uondoe mali zako kwenye eneo la hifadhi ya barabara katika kipindi cha siku 90 baada ya siku hizo kwisha tutaingia katika ardhi hiyo na kuanza kazi ya ujenzi bila ya taarifa yotote," inasomeka sehemu ya barua hiyo kumb. Namba VAL/TRD/MAW ya Julai 18 mwaka huu iliyosainiwa na Meneja wa TanroadsMkoa wa Dodoma, Leonard Chimagu.
Wameiomba Serikali kuangalia fidia hiyo kwani ni haki yao ni si vizuri kwa mamlaka husika kuamua watakavyo; ni sivyo inavyostahili kuwa.
Akizungumzia kwa njia ya simu jana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Rehema Nchimbi alisema si dhambi wananchi hao kudai haki yao inayoonekana kutotendewa haki kwa kazi zima ya malipo ya fidia hiyo.
"Mtazamo wa waliolipwa unaweza kuonekana kuwa malipo hayo si halali, lakini kwa upande mwingine, malipo hayo yanaweza kuwa halali kutokana na vigezo vilivyotumika lakini jambo la msingi hapa ni kufahamu kuwa hawa walitathmini, waliolipwa wote ni binadamu na wanaweza kukosea," alisema Dkt. Nchimbi.
Aliongeza kuwa jambo la msingi ni jamii kwa ujumla waangalie manufaa ya barabara hiyo ya kiwango cha lami itakapokamilika kwamba ni makubwa, Kondoa, ndiyo ilikuwa kiongozi wa wilaya nyingi nchini, haikuwa na njaa, ilikuwa nzuri kiuchumi ikilisha mikoa yote ya kaskazini, ni wakati sasa wa kuirudishia heshima yake ya awali badala ya kulumbana.
Alionya kuwa suala hilo lisichukuliwe na watu wengine kama mradi wao kwa kuwachochea wananchi kwa lengo la kukwamisha mradi usitekelezwe kwa wakati, lishughulikiwe kwa kutumia busara na hekima ili wananchi hao wasikose haki yao na mradi huo utekelezwe.
Sakala la fidia kwa wananchi hao limesababisha ujenzi wa barabara hiyo kutoanza kwa takribani mwaka mmoja, baada ya Serikali Mkoa wa Dodoma kugoma kuwalipa fidia wakazi wa maeneo ya barabara hiyo waliyojenga kwenye hifadhi hadi wafadhili Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Misaada ya Japan (JICA) walipoingilia mvutano huo na kuamuliwa lazima wananchi hao walipwe stahili zao

No comments:

Post a Comment