20 August 2013

WANANCHI WAKABIDHI ARDHI KUJENGA CHUO



Na Esther Macha, Mbeya
WAKAZI wa Kijiji cha Lukata Kata ya Kinyara, wilayani Rungwe mkoani Mbeya wamekabidhi ardhi kwa hospitali teule ya Igogwe kwa ajili ya kujenga chuo cha uuguzi katika hospitali hiyo ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya. Imeelezwa kuwa wananchi wa kijiji hicho wamekabidhi ardhi hiyo kwa hospitali yenye ukubwa wa ekari zaidi ya tano ili chuo hicho kianzwe kujengwa mapema.

Tukio hilo limefanyika katika eneo lililopo jirani na hospitali hiyo ambapo Katibu wa Hospitali ya Kalindu, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Mwakanosya na viongozi wengine wa serikali na kupita maeneo yote kuweka alama. Makabidhiano hayo yamefanyika baada ya Askofu Chengula kutoa kilio chake wakati wa Jubilee ya fedha ya miaka 50 tangu kufunguliwa kwa Hospitali ya teule ya Wilaya ya Igogwe.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa makabidhiano ya eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela alisema baada ya kusikia mahubiri ya Askofu huyo kwa uchungu aliona ipo sababu ya kufanya haraka kufuatilia suala hilo na kulikamilisha na hivyo kupitia nyaraka za awali.
Alisema kupata matokeo ya tume ya uchunguzi iliyoundwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Rungwe aliamua kutoa ardhi kwa niaba ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ndiye mwenye ardhi kikatiba.
"Nyaraka zilionesha kuna ubabaishaji mwingi kwa sababu taratibu zote za kutuma maombi zilifuatwa kuanzia ngazi ya Kijiji, nikaona Rungwe tuna upungufu wa wauguzi 128, nikaona chuo kitakuwa mkombozi katika zahanati na vituo vya afya ambavyo vina upungufu mkubwa wa wataalamu kwa hiyo ninakukabidhi ramani hii Baba Askofu anzeni mara moja kujenga baada ya Desemba 22 watakapokuja watu wa upimaji na ahadi ya watoto wa kijiji hiki na Rungwe kwa ujumla kupewa kipaumbele usisahau," alisema.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa anao mzigo mkubwa wa wanafunzi zaidi ya 4,000 kati ya 5,000 waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ambao wapo wanazurura mitaani baada ya kuchaguliwa wanafunzi 800 kati yao kuendelea na kidato cha tano.
Askofu Chengula ameishukuru serikali na kumtaka Mkuu wa wilaya kufikisha salamu zake kwa serikali ya Wilaya, kwa Mkuu wa Mkoa na Rais Jayaka Kikwete kwa kumkabidhi ardhi hiyo kwa ajili ya manufaa ya Watanzania kwani wataalamu watakaosoma hapo watakuwa ni watoto wa Watanzania.
Akisoma risala mbele ya mkuu wa wilaya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Igogwe, Dkt. Oyeti Mwakosya alisema chuo kinatarajia kuanza na wanafunzi 90 wa ngazi ya cheti kutokana na mipango ya serikali na wanatarajia kuendelea kutoa kozi za ngazi ya stashahada na shahada kwa wauguzi na kwamba ujenzi wa chuo ni faraja kwa Wilaya na Jimbo Katoliki la Mbeya.
Chifu wa Kijiji cha Lukata alimshukuru Askofu Chengula na Mkuu wa wilaya kwa kushirikiana nao kuhakikisha ardhi hiyo inapatikana kwani uwepo wa chuo hicho ni bahati kubwa kwao na kwamba watu wake wote wamepokea tukio hilo la kihistoria kwa furaha na ndiyo maana wamejitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la Askofu kukabidhiwa rasmi ardhi ambapo zaidi ya machifu 12 walishiriki.


No comments:

Post a Comment