25 July 2011

Mgeja naye amkaba koo Sitta

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

SAKATA la malumbano kati ya viongozi wakuu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) limeendelea kupamba moto baada ya mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa
Shinyanga, Bw. Hamisi Mgeja kuungana na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. John Guninita kumtuhumu Bw. Samuel Sitta juu ya kauli zake dhidi ya serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga jana, Bw. Mgeja alisema kauli zinazotolewa na Bw. Sitta ambaye pia ni waziri wa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kuwa chanzo kikubwa cha kukisambaratisha Chama cha Mapinduzi.

Kauli ya Bw. Mgeja ambaye pia ametoa ushauri kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kukaa nakuangalia njia muafaka itakayomuwezesha Bw. Sitta arudi katika mstari kwa kuheshimu
katiba na kanuni za chama, imekuja siku chache baada ya viongozi wengine wawili wa CCM kutoa shutuma kama hizo dhidi yake.

Wa kwanza kumlaumu Bw. Sitta alikuwa Naibu Waziri wa mambo ya Ndani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, akafuatiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. John Guninita ambao kwa nyakati tofauti waliwatupia lawama Bw. Sitta na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye.

Lakini Bw. Sitta alijibu mapigo hayo kwa mkupuo akisema ataendelea kusema ukweli na kamwe hawezi kubabishwa na mawakala wa mafisadi.

Kama ilivyokuwa kwa wenzake, Bw. Mgeja alimtaka Rais Kikwete 'ampige pini' Bw. Sitta ili aweze kutumia vikao pale anapoona mapungufu yoyote yanayofanywa na chama au serikali yake badala ya kushambulia akiwa nje majukwaani.

Kauli za Bw. Sitta za kuikosoa serikali na CCM alizitoa katika mkutano wa hadharani mjini Mbeya ambao mgeni rasmi alikuwa Bw. Nnauye, ambapo kiongozi huyo alikosa watendaji wa serikali, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja kwa kushindwa kupata suluhisho la mgawo wa umeme.

Bw. Mgeja alisema kauli za Bw. Sitta zinaonesha wazi zinaashiria aina ya uchochezi uliofichika ambao usipodhibitiwa mapema kuna hatari ya kukibomoa chama na hivyo hazistahili kuvumiliwa kwa vile ni sawa na usaliti unaoweza kusababisha mapinduzi baridi kwa
serikali iliyoko madarakani.

"Kwa kweli hizi kauli za mwenzetu Bw. Sitta hata mimi nazipinga vikali, na naungana na mwenzangu wa Bw. Guninita kuhisi kwamba huenda mwenzetu huyu anatumika vibaya kwa lengo la kutaka kukigawa Chama chetu," alisema.

Aliongeza: "Nafikiri lengo ni kutaka kuwepo kwa mapinduzi baridi ndani ya serikali ya CCM, na ikizingatiwa kuwa yeye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri katika serikali hii ya awamu ya nne, ambaye ki-utaratibu alipaswa kutoa majibu sahihi ya mapungufu yote
ndani ya serikali na kuitetea badala ya kukaa pembeni na kulalamika.

Bw. Mgeja alifafanua kuwa waziri yeyote anastahili kuwa upande wa serikali pale anapokuwa kwa wananchi, kinyume na jinsi anavyofanya Bw. Sitta ambapo hivi karibuni wakati akiwa mkoani Mbeya aliwaacha wananchi pasipo majibu ya matatizo yao na yeye kubakia kuwa mmoja wa walalamikaji.

Hata hivyo, Bw. Mgeja alikiri kwamba hivi sasa baadhi ya Watanzania
mmoja mmoja wameathirika kiuchumi pamoja na taifa kwa ujumla katika suala zima la kimapato kutokana na tatizo la uhaba wa umeme nchini na kwamba jambo ambalo Bw. Sitta hakupaswa kujitoa na kuilaumu serikali.

"Ni unafiki mkubwa na uasi kwa waziri aliye ndani ya serikali kuishutumu serikali yake na kuishinikiza iwaombe radhi wananchi katika mkutano wa hadhara badala ya kutumia hekima kushauri suala hilo kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri ambavyo mwenyekiti wake ni Rais Jakaya Kikwete.

"Ni kweli matatizo ya nishati ya umeme yameathiri kwa kiwango kikubwa taifa, lakini alipokuwa huko Mbeya hakustahili kutoa kauli zile za kinafiki, kuitaka serikali iombe radhi katika mkutano wa hadhara, hili ni tatizo tena waziri Sitta hakutumia busara, kama anaiona nyumba aliyomo ina matatizo kwanini aendelee kuishi?" alihoji Bw. Mgeja.

Pamoja na tuhuma hizo, Bw. Mgeja alikiri kuwa kauli za Bw. Sitta ni changamoto kubwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuhakikisha kinanusuru hali hiyo kwa kumdhibiti, waziri huyo juu ya kauli zake hizo zisizo na nia njema na CCM na serikali yake kwa ujumla.

"Namuomba Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Bw. Mukama (Wilson) azitazame kauli hizo kwa macho mawili, kwani adui wa ndani ni mbaya sana kwa ustawi wa maendeleo, kama jinsi zinavyoonekana kauli za Bw. Sitta ambazo zina dhamira ya kutengeneza makundi ndani ya Chama kwa kubainisha kundi bora na lisilo bora," alieleza Bw. Mgeja.

9 comments:

  1. nami naungana na Mhe. Sitta kutetea kauli ile

    ReplyDelete
  2. Kuna msemo wa pwani niliwahi kuambiwa siku za nyuma kuwa NGOMA YA MAJINI IKIPIGWA WENYE MARUHANI WOTE HUWEWESEKA! Hapa naona wanaweweseka tu, mimi nashauri hata hao waandishi wakiitwa kwenye vikao vyaaina hii wakifika waeme vifaa vyao vyakurekodia havina chaji ili watu kama huyu mgeja wajue uzito wa tatizo na watie akili. Ni hayo tu

    Mtanzania aliye gizani

    ReplyDelete
  3. Sokoine's Cousin!

    Kama late Sokoine angukuwepo nadhani Rais wa TZ angekuwa Hon. Samuel Sitta! Prime Minister angekuwa Magufuli bila kupinga! Lakini kwa bahati mbaya kabisa, kabisa!!! Tunaongozwa na bongo flavor JK, ambae hana tofouti hata kidogo na bongo flavor, bongo movie, simba, yanga!

    ReplyDelete
  4. Tatizo kubwa hapa ni watu kutopenda ukweli na kuegemea uongo, mtu akisema kweli anaonekana ni tatizo. Sitta hapashwi kulaumiwa kwa kuona tatizo na kuwaambia watanzania ukwel, huwezi ukafunika mambo eti kwa sababu na wewe ni mhusika.SITTA endelea kuwa mkweli na MUNGU atakutetea yeye anasema hata mwacha mwenye haki wake adhirike, hautaadhirika kamwe kwani MUNGU atakuwa nawe na watanzania wamekuzunguka nyuma mbele , kushoto na kulia kwako.

    ReplyDelete
  5. CCM haielewani. Hata UVCCM hawaelewani. CHADEMA. wanaelewana.

    Tunamtaka Dr. Slaa na mchumba wake Josephine waongoze nchi. Kwanza bw. Sitta si CCM. yeye ni CCJ

    ReplyDelete
  6. Sitta ni CCJ au ni CCM? Ni dhahiri kua ni CCJ. Anataka aivuruge CCM badae arudi kuimarisha CCJ.

    Wakati huo itakua ni CCJ na CHADEMA.

    Achaneni ni na Sitta. Ni mnafiki. Huyo ni CCJ na ndio hao hao.

    2015 chagua kati ya Mbowe. Slaa, Zitto na Lissu

    ReplyDelete
  7. ""Ni kweli matatizo ya nishati ya umeme yameathiri kwa kiwango kikubwa taifa, lakini alipokuwa huko Mbeya hakustahili kutoa kauli zile za kinafiki",
    kwa kauli ya MGEJA hapo juu ni nani mnafiki sitta anayezungumza ukweli au yeye mgeja anayesema kuwa hakustahili kusema pamoja na kwamba hiyo ni kweli. mgeja wewe ni mnafiki kwa kuendeleza siasa za kizamani za kuwadanganya watu kama watoto wadogo.

    ReplyDelete
  8. Eng. mwakapango,E.P.AJuly 25, 2011 at 10:31 PM

    Kiongozi wa wananchi siku zote anatakiwa kuwa na nidhamu na kuheshimu madaraka aliyopewa ili aweze kuwatumikia vema watu wake. kusema ukweli na kutetea maslahi ya wananchi haiondoi dhana ya kuwa na nidhamu. kiongozi mtovu wa nidhamu hata akipewa madaraka anaweza kugeuka kuwa dictator na akasababisha madhara makubwa kwa wananchi. Samwel Sitta alikuwa spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haingii akilini yeye kukubali cheo kidogo kabisa cha uwaziri wa Afrika mashariki na kuwa anaripoti kwa naibu spika wake nadhani kuna kila dalili za samwel sitta kuwa power monger. amepewa platform ya uwaziri kutoa kauli za kubeza serikali na mawaziri wengine ni kujaribu kumchonganisha mheshimiwa Raisi na wananchi waliomchagua. Watanzania wenzangu mwenye macho aambiwi tazama juzi tu Samwel sitta amethubutu kubeza wapinzani kuwa wanaongea lugha nyepesi nyepesi na ni wanafiki. mambo yote anayopita kuongea yeye Sutta ndiyo sera za wapinzani. wapinzani hawaongei lugha nyepesi nyepesi mzee wanaongea mambo ya kitaifa kama vile EPA , Richmond,rushwa ya rada na kama unataka kufanya vizuri toka huko usisingizie kuwa ulikuwepo tokea shule ya sekondari. naomba nimshauri Raisi wangu Mpendwa Dr. JAKAYA MLISHO KIKWETE AMFUKUZE KAZI SAMWELI SITTA ILI ARUDI CCJ. nikifanikiwa kuonana Raisi ilo ndiyo jambo zuri pekee kabisa naweza kumwomba. vilevile naomba nimshauri sitta kama senior parlamentarian ajiuzulu uwaziri ili aweze kuwa mkweli zaidi. KAMA AMEACHIWA TU SIKU TATU NA PINDA KUKAIMU NAFASI AKANYANYASA WAPINZANI AKIWA RAISI SI ATAPIGA RISASI. Hatufai diktata mkubwa huyu ANATAKA KUTUHARIBIA NCHI.

    ReplyDelete
  9. Matatizo yote haya yanakuja kwa sababu ya kuwa na rais asiyekuwa na sauti mbele ya viongozi wa chini yake.Hawezi kukaa nyumbani kwake na kufikiri jinsi ya kutatua matatizo yanayoikabili nchi yake,kila siku yeye ni mguu na njia kwenda kutembea kwa wenzake na kujidai yakuwa anatafuta wawekezaji wanao kuja kuwekeza gizani.Labda tumuulize raisi wetu kama hao wawekezaji wanakuja kuwekeza kwa solar system.Na je huko anakokwenda kila siku amejifunza nini?.Au kazi yake ni kufuja pesa za walipa kodi.

    ReplyDelete