26 July 2012

Chakula chenye sumu chaua mmoja, wengine mahututi


Na Eliasa Ally, Iringa

MKAZI wa Kijiji cha Ibofye, Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa Bw. Faruni Nyaupumbwe (65), amefariki dunia na wengine zaidi ya 10 wamelazwa katika Hospitali za Mkoa wa Iringa na Kituo cha Afya Ihambo baada ya kula chakula chenye sumu katika sherehe.


Wakizungumza na Majira jana, wahanga hao walisema tukio hilo limetokea juzi baada ya mkazi wa kijiji hicho Bw. James Ngaile, kuandaa chakula na kinywaji aina ya togwa kwenye sherehe za kuoza binti yake.

Walisema baada ya kula chakula na kunywa, walirudi majumbani mwao na ilipofika usiku, waalikwa wengi waliokula chakula hicho walianza kuarisha hivyo walilazimika kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kijiji ambaye naye alikuwa hajiwezi kutokana na kula chakula hicho.

“Kutokana na hali hiyo, uongozi wa kijiji ulilazimika kukodisha gari ili kupeba waathirika zaidi ya 15 na kuwapeleka Kituo cha Afya Ihimbo, baadhi yao hali zao zilikuwa mbaya na kukimbizwa Kituo cha Afya Ipogolo, wengine Hospitali ya Mkoa,” walisema.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Bw. Godfrey Mtete, alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji hicho lakini hadi sasa haijulikani kama tatizo lilikuwa kwenye chakula, mboga au togwa.


Alisema idadi ya wananchi waliopatwa na tatizo hilo wapo 15 na zaidi ya 13 wapo mahututi. Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamhanda, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa, mtu mmoja Bw. Faruni Nyupumbwe, amefariki dunia katika sherehe hiyo ambapo watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment