Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), wakiwa kwenye viwanja vya ofisi za mamlaka hiyo, Dar es Salaam jana, wakati wa mgomo unaotokana na kutolipwa mishahara ya miezi 4 mfululizo kuanzia mwezi Mei.
Rehema Maigala na Darlin Said
SAKATA la
mgomo wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA),
limeendelea kuchukua sura mpya ambapo jana wameendelea na mgomo wakitaka Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda aende kusikiliza madai yao.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Chama cha
Wafanyakazi wa Reli katika shirika hilo (TRAWU), Erasto Kihwele alisema
wanamtaka, Pinda aende kusikiliza kilio chao ili mgogoro huo upate suluhisho la
kudumu.
Alisema, hadi sasa wana miezi minne hawajalipwa mishahara
na hawajui lini watalipwa ili waweze kujikimu kimaisha. "Sisi tunaendesha treni ambayo inapakiza roho za
watu, hatuwezi kuendesha tukiwa na njaa, mawazo tunaweza kusababisha ajali
njiani," alisema Kihwele.
Aliongeza kuwa, shinikizo la kugoma limeanza wiki
iliyopita, lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa, hivyo hakuna usafiri
wowote wa treni itakayoondoka eneo hilo.
Alisema, wafanyakazi wana mpango wa kukesha TAZARA ili Waziri Pinda
akifika aweze kuwakuta na kueleza kilio chao. "Si wafanyakazi wa Dar es
Salaam pekee ambao tumegoma bali hata wale wa Tunduma," alisema.
Kihwele alisema, sababu za wao kutolipwa mishahara ni mikataba mibovu
dhidi ya Serikali ya Tanzania na Zambia kwani asilimia 70 kati ya 100,
inakwenda Zambia ambapo Tanzania inabaki asilimia 30 ambayo haiwezi kuendesha
shirika. Sababu nyingine ni uzembe wa viongozi kutofuatilia madeni wanayodai.
Naye mjumbe wa Chama cha Usafirishaji nchini, Mwenevyale Juma alisema,
kama Serikali haitawasikiliza wafanyakazi hao, watatoa shinikizo la kusimamisha
shughuli zote za usafirishaji nchini.
Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya majina yao
kutoandikwa gazetini, walisema walikata tiketi ili waweze kuondoka Ijumaa wiki
iliyopita lakini hadi jana walishindwa kuondoka kwa sababu ya mgomo huo
No comments:
Post a Comment