Na Salim Nyomolelo
SHIRIKA la
Maendeleo na Uwekezaji la Alhayat kutoka nchini Oman litatumia dola za
Kimarekani milioni 100 kuwekeza katika Shirika la Ndege nchini (ATCL), sambamba
na kujenga jengo la ghorofa 25 katika eneo la Posta jijini Dar es Salaam kama
serikali ikiridhia kusaini mkataba nao.
Shirika hilo lilifanya ziara Dar es Salaam jana katika
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) ili kujionea fursa zilizopo pamoja na
changamoto kwa lengo la kuwekeza.
Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara hiyo,
Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Shekhe Salim Bin Abdullah
alisema kuwa wamepania kuwekeza ATCL ambapo wataingiza ndege nane za kisasa
mara baada ya kukubaliana na serikali ikishapitia rasimu ya mkataba.
Shekhe Abdullah alisema kuwa, licha ya kuwekeza ATCL, pia litaboresha
miundombinu pamoja na kuweka vifaa vya kisasa katika uwanja huo ili kuboresha
usalama kwa wateja.
Alisema kuwa, shirika limepania pia kujenga jengo kubwa la kisasa katika
eneo la Posta ambalo litakuwa na ghorofa 25 na kuongeza kuwa huduma mbalimbali
zitakuwepo ikiwa ni pamoja na Supermarket ambayo itakuwa kubwa hapa nchini,
maduka mbalimbali, hoteli, huduma za simu, maeneo ya maegesho ya magari pamoja
na ofisi za shirika la ndege.
"Ili kwenda sawa na mfumo huo, tutachukua baadhi ya wafanyakazi
kuwapeleka Oman kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimbali ya kisasa, hasa katika
utoaji wa huduma wa viwanja vya ndege ambao nao watatoa mafunzo kwa
wenzao," alisema Shekhe Abdullah.
Alisema kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kujenga mazingira kwa ajili ya
kuwapata na kuwavutia wateja ili kupanua wigo wa kutoa huduma bora na si
kufanya kazi kiholela jambo ambalo litasababisha wateja kukimbia.
Hata hivyo, miongoni mwa mapendekezo aliyotoa Shekhe Abdullah ni pamoja
na kuongeza kamera za kisasa zenye uwezo mkubwa, kuboresha kitengo cha zimamoto
na uokoaji, kuboresha hali ya usalama ili kuepukana na upotevu wa mizigo ambao
unaweza kujitokeza pamoja na vifaa vya kisasa vya kukagulia mizigo ambapo wakishaingia
mkataba na serikali atasaidia kuviweka.
Alisema kuwa, ziara aliyoifanya Rais Jakaya Kikwete nchini Oman hivi
karibuni iliwavutia kuja kuwekeza baada ya kukaribishwa wafanyabiashara ambapo
aliongeza kuwa Tanzania na Oman zina historia nzuri pamoja na kuunda undugu
kutokana na kuoana.
Kwa upande wake Waziri wa
Uchukuzi Dkt. Harisson Mwakyembe alisema kuwa, Serikali itapitia rasimu ya
mkataba huo kwa kina kabla haijaingia makubaliano ya shirika hilo licha ya wao
kuwa na nia nzuri ya kuwekeza.
.."Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harisson Mwakyembe alisema kuwa, Serikali itapitia rasimu ya mkataba huo kwa kina kabla haijaingia makubaliano ya shirika hilo licha ya wao kuwa na nia nzuri ya kuwekeza.".. Hapo Mwakyembe umesema maana Oman si kama wameendelea katika huduma na biashara za ndege,Oman air haina sifa nzuri kiusalama duniani,sasa leo wachukuwe watu wakajifunze kwao kwanini?nsi heli tupeleke watu Ethiopia au Qatar?Katika enzi hizi za utandawazi watanzania tusiwe wavivu wa kufanya research za haraka haraka kwenye mtandao,tusitegemee elimu darasa tu,huu ni wakati tofauti.Nimejaribu kupata jina la kampuni na la mkubwa wao alietajwa humu kwenye mtandao nikaambulia patupu.Hapa ina maana mwandishi hakuhakiki kupata majina sahihi au ndio mambo ya richmond ya kampuni za briefcase.
ReplyDelete