29 January 2013
TRA yatakiwa kutafuta mbinu mpya ya ukusanyaji kodi
Na Mariam Mziwanda
NAIBU Waziri wa Fedha na Uchumi Bi.Saada Mkuya ameitaka Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kutafuta mbinu mpya za ukusanyaji wa kodi ili kuliongezea taifa mapato.
Bi.Mkuya aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mahafali ya tano ya Chuo cha Uhasibu (TIA) na kusisitiza haja ya mamlaka hiyo kutumia taasisi zake katika kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa kila ngazi ya jamii.
"Tunaitaka TRA waendelee kuimarisha chuo na kuhakikisha kila mwanachuoni anayehitimu anakua balozi katika familia na jamii kwa kueneza elimu ya kulipa kodi na umuhimu wake ili kila mwananchi ajue kuwa ni wajibu wake kwa maslai ya taifa,"alisema.
Alisisitiza wahitimu hao kutumia taaluma hiyo kwa kuwa wabunifu wa somo la maadili na kuwa waaminifu katika kazi zao ili taifa liweze kufikia malengo kwani ongezeko la wataalamu wa kodi ni changamoto kwa Serikali kutokana na mahitaji yaliyopo kwani umuhimu wa walipa kodi kupatiwa huduma ni mkubwa.
Aliutaka uongozi wa chuo hicho kudumisha ushirikiano na vyuo vya Bara la Afrika ili kuendeleza matunda ya vijana kuajiliwa katika nchi mbalimbali huku akiwataka kupanua wigo wa elimu na kuweza kuwafikia nchi nyingi duniani sambamba na kutekeleza mkakati wa uboreshaji wa eneo jipya la ujenzi wa chuo huko Kibaha na mikoani.
Aliitaka TRA kutokuridhika na kiwango cha ukusanyaji wa kodi cha Sh.trilioni 8 kwa mapato ya ndani kwa mwaka ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo ya kuondokana na bajeti ya utegemezi kwa wahisani na kuitaka mamlaka hiyo kushirikiana na Serikali katika kuchukua hatua kwa kuhakikisha inaondoa malalamiko ya wananchi ya kuwepo maafisa walipa kodi wasio waadilifu.
Naye Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho Pro. Palamagamba Kabudi alieleza kuwa kati ya wahitimu 435 waliotunukiwa cheti miongoni mwao wanawake ni 137 na 298 wanaume ambapo wafanyakazi 33 ni kutoka TRA na nane wakiwa ni maofisa forodha kutoka Botswana.
Alisema jumla ya wahitimu 186 walitunukiwa cheti cha uwakala wa forodha cha Afrika Mashariki,98 cheti cha usimamizi wa forodha na kodi huku 88 kati yao wakipatiwa stashahada ya usimamizi wa forodha na kodi na wengine 63 wakipatiwa stashahada ya uzamili katika kodi.
Alisema kuwa chuo hicho kinajivunia uanzishwaji wa kozi ya stashahada ya uzamili inayoitwa master of arts in Revenue law and Administration kwa ushirikiano na chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo Kikuu cha Munster huko Ujerumani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment