29 January 2013
Wakulima wa kahawa watuhumiana K'njaro
Na Gift Mongi
MRAJISI Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Kilimanjaro, Kasya Kasya amedaiwa kukikingia kifua Chama Kikuu cha Ushirika mkoani humo (KNCU) ikiwemo kulihujumu zao la kahawa.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa Oktoba 24, mwaka jana kutoka Chama cha Msingi Marangu Mashariki ambayo mwandishi wa habari hizi ana nakala yake
ilitaka mrajisi huyo kukiruhusu chama hicho kukopa sh. milioni 10 katika Benki ya KCB kwa ajili ya kununulia pembejeo lakini hawakuruhusiwa.
Barua hiyo iliyoandikwa na Mwenyekiti wa chama hicho cha msingi, Charles Lyimo kuomba kukopeshwa kiasi hicho cha fedha ilieleza kuwa KNCU haina fedha kwa ajili ya kuwasaidia wakuliam kununulia pembejeo.
"Madeni tunayodai KNCU ni masawazisho ya bei ya kahawa sh. 500 kwa kila kilo kwa msimu 2011/2012 ambayo ni kilo 40,241. Ambapo hapa ni zaidi ya milioni 20,"ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Pia maelezo katika inaendelea kufafanua kuwa, kutokana na ukata unaoikumba KNCU wameshindwa kulipwa mabaki yao hivyo kukosa fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo za kuendeleza zao hilo la kahawa.
Hata hivyo wakulima hao kupitia barua yao hiyo walikiri kuwa KNCU ina duka la pembejeo ambalo haliwakopeshi wakulima na badala yake huwauzia bei ghali.
Aidha, kutokana na hali hiyo Mrajisi Msaidizi huyo inadaiwa alikikataza chama hicho kukopa fedha kwa madai kuwa deni limefika kikomo wakati KNCU ina madeni lakini bado wanaruhusiwa kukopa.
Barua ya Mrajisi Msaidizi yenye kumbukumbu namba BD 54/247/04/K ya Desemba 31, 2012 imetaka chama hicho cha msingi kuhudumiwa na KNCU kwa kuwapatia mahitaji yote ikiwemo pembejeo katika duka la chama hicho.
"Mrajisi huyo akijua fika kuwa KNCU ina madeni alikitaka chama cha msingi kihudumiwe na KNCU mahitaji yake yote, ingawa tayari KNCU ilishindwa kulipa mabaki ya wakulima hao.
"Je hakuna madeni yoyote mnayodaiwa na KNCU (1984)LTD? Tafadhali kuweni wawazi kwani wao ndio wenye mamlaka ya kuwahudumia," iliongeza sehemu ya barua hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Mrajisi huyo alidai hana lengo la kuitetea KNCU na badala yake mahesabu yake ndio yatakayojieleza na si vinginevyo.
"Ndugu naomba unielewe KNCU sina njama nao hata kidogo ila mimi ninachokijua mahesabu yao ndio yatakayojieleza kaka," alidai Mrajisi huyo.
Katika mkutano mkuu maalumu ulioitishwa mapema Januari mwaka huu, uliolenga kujadili kushuka kwa zao la kahawa Mkoa wa Kilimanjaro uliahidi kulipa mabaki ya wakulima ifikapo tarehe 15 mwezi huu jambo ambalo hadi hivi sasa halijatekelezeka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment