01 August 2012

Wafanyakazi NICOL wailalamikia CMSA, mifuko minne ya pensheni



Na Mwandishi Wetu

WAFANYAKAZI wa Kiwanda cha Samaki NILOL, jijini Mwanza (TFDC), wamelalamikia kitendo cha Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA) pamoja na mifuko minne ya pensheni nchini kwa kuwaweka katika maafa makubwa, kuvunja sheria na kuhujumu uendeshaji wa Kampuni ya Taifa ya Uwekezaji.


Taarifa ambazo gazeti hili imezipata Dar es Salaam jana, zinasema mbali ya CMSA, mifuko inayolalamikiwa ni Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Watumishi wa Umma (PSPF), Serikali za Mitaa (LAPF) na Watumishi wa Serikali (GEPF).

Inadaiwa kuwa, Julai 9 mwaka huu, wafanyakazi 26 wa TFDC, walifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam yenye namba 15,2012 dhidi ya CMSA na mifuko hiyo kwa ukiukaji katiba na kusababisha washindwe kupata mishahara yao.

Katika kesi hiyo, wafanyakazi hao wanataka mifuko hiyo ya kiserikali iheshimu katiba na haki za wafanyakazi badala ya kuwanyima haki zao za msingi ambazo zimewekwa wazi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

Walisema mifuko hiyo imekwenda mahakamani na kusimamisha malipo ya mishahara yao wakidai kulinda fedha zao zilizopo NICOL hivyo kusababisha maisha yao kuwa magumu.

Kutokana na hali hiyo, wafanyakazi hao wanaiomba mahakama hiyo iamuru mifuko hiyo imlipe kila mfanyakazi sh. milioni 50 na sh. milioni 100 kama adhabu na malipo mengine ambayo mahakama itaamua kutokana na ukatili, matumizi mabaya ya ofisi za mifuko na nia mbaya ambavyo vimesababisha ukali wa maisha kwa wafanyakazi hao.

Inaelezwa kuwa, mwanzoni mwa 2010, NICOL ilisitisha uzalishaji katika kiwanda hicho ili ifanye tathmini upya kuhusu masoko ya kiulimwengu na kuweka mikakati.

Madai ya wafanyakazi hao yanaonesha kuwa, NICOL iliendelea kuwalipa mishahara wakati uzalishaji ulipositishwa kwa sababu walikusudia kukirudisha kiwanda katika uzalishaji.

Mwishoni mwa 2010,  kiwanda hicho kilianza tena kupata oda za mauzo ya nje dola za Marekani milioni 32 lakini mamlaka yenye nguvu, zilitumia nafasi zao kuhakikisha mauzo hayo hayafanyiki.

Madai hayo yaanaeleza kuwa, wafanyakazi walipata taarifa kuwa CMSA iliiamuru NICOL isiweke fedha katika kiwanda hicho, kufukuza Bodi na Menejimenti pamoja na kufunga akaunti za kampuni hiyo kwenye benki zote nchini.

Wafanyakazi  hao pia wanadai kuwa, Septemba 2011 baada ya kupeleka madai yao Mahakamani ya Kazi, iliamuliwa walipwe na TFDC ambapo NICOL kwa kutambua hiyo ni haki yao haikuwa na pingamizi lolote lakini CMSA ilizuia.

Januari 2012, nyaraka zilizopo mahakamani zinaonesha sh. milioni 65 za kuwalipa wafanyakazi hao, zilihamishwa kutoka akaunti ya NICOL ya NMB na kupelekwa Mahakama ya Kazi tayari kwa malipo hayo.
Inaelezwa kuwa, CMSA na mifuko hiyo walikwenda mahakamani kuzuia wafanyakazi wa TFDC wasilipwe na kuwasilisha mashtaka ambayo yanachangia ucheleweshaji malipo ya wafanyakazi kwa miezi 18 na kuwafanya kuwa ombaomba.

Machi 2013, Mahakama ya Kazi ilitoa hukumu kwamba CMSA walivunja sheria kwa kuiondoa Bodi na Menejimenti ya NICOL pamoja na kuzuia kutumika kwa akaunti za kampuni hiyo.

Katika hukumu hiyo, mahakama iliamuru wote walioondolewa warudi kazini na kufunguliwa akaunti za NICOL.

Madai mengine yaliyotolewa na wafanyakazi hao ni watendaji wakuu CMSA na mifuko hiyo, kulipwa na fedha za umma ambazo zinatokana na michango ya wafanyakazi, kupokea mishahara mikubwa, kutumia magari ya kifahali na watoto wao kusoma kwenye shule nzuri na zenye gharama kubwa ndani na nje ya nchi.

Wafanyakazi hao waliongeza kuwa, fedha za umma za wafanyakazi pia zinatumika kuwalipa mawakili ili wazuie haki yao mahakamani na kusababisha zichelewe.

Inadaiwa kuwa, wafanyakazi waliofungua kesi mahakamani wengi wao wamepoteza makazi waliyokuwa wakiishi na familia zao na wengine hawana chakula na kukosa ada za watoto wao.

No comments:

Post a Comment