01 August 2012

Ukweli unafichwa tuhuma za rushwa bungeni –CCM



Darlin said na Agnes Mwaijega

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimelaumu juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, alisema zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa ajili ya kutaka kujitangaza.


"Mfano mzuri wa juhudi hizo ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni  mbunge wa CHADEMA na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kutoa orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndiyo watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa," alisema, Bw. Nnauye na kuongeza;

"Inashangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa CHADEMA, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii”.

Bw.Nnauye alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zina lengo la kuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana CHADEMA.

“Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti,” alisema

Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika haitoshi kuwaita walarushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.

"Wakithibitika kali zichukuliwe kulikomesha kabisa tatizo hili na iwe fundisho kwa wengine,” alisema Bw. Nape.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) Dkt. John Malecela amesema haungi mkono vitendo vya rushwa ambavyo vinafanywa na baadhi ya wabunge.

Alisema kama itathibitika kuwa tuhuma za rushwa zinazowakabili wabunge ni za kweli, wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria, bila kujali vyama wanavyotoka.

Dkt. Malecela alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati akitoa maoni yake kwa waandishi wa habari kuhusu sakata la baadhi ya wabunge kuhusishwa na rushwa.

2 comments:

  1. Nape tulia acha vyombo husika vifanye kazi yake kisha itajulikana nani kala rushwa kama wa ccm au wa cdm kisha wananchi tutajua cha kufanya.

    ReplyDelete
  2. UADILIFU KAMA ILIVYO UBAGUZI WA RANGI HAUTOFAUTISHWI KWA MACHO NI MAADILI NDANI YA MTU INAUMA LAKINI INABIDI KUKUBALI UKOSEFU WA MAADILI UKO NDANI YA MTU HAUONEKANI KWA MACHO UKWELI UKIDHIHIRIKA WANAOZUNGUMZA BILA KUTAFAKARI,WANAOTUMIA VICHWA KUFUGA NYWELE BADALA YA KUFIKIRI WATANYAMAZA

    ReplyDelete