01 August 2012
Grand Malt, ZFA watoa pole Zanzibar
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Zanzibar, ambao ni kinywaji kisicho na kilevi cha Grand Malt, wametoa mkono wa pole kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikiwa ni kiasi cha sh. milioni 5, kwa ajili ya waathirika wa ajali ya boti ya MV Skagit, iliyotokea hivi karibuni.
Akikabidhi pole hiyo kwa Makamu wa Pili wa SMZ, Balozi Seif Idd, Meneja Masoko wa Grand Malt, Fimbo Butallah alisema wameguswa na tukio hilo na wameamua kuungana na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu.
“Tumeguswa na tukio hili na Grand Malt ambao tuko hapa Zanzibar kama wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya hapa, tumeamua kuungana nanyi katika kipindi hiki kigumu.
“Tunapenda kuwapa pole waliofiwa na wale wote waliokuwemo katika boti hiyo na kwa ujumla kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla,” alisema.
Naye Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam alisema walishitushwa baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo na kuamua kuungana na wengine katika kutoa pole yao.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Kassim Suleiman naye alisema walishitushwa pia na ajali hiyo, kwani wamepoteza watu ambao walikuwa mhimili mkubwa katika maendeleo ya mchezo huo visiwani.
Balozi Idd, aliwashukuru Grand Malt kwa pole yao na kusema atafikisha salamu zao kwa wahusika na kuitaka pia iendelee kuwa na moyo huo wa kusaidia pia michezo ndani ya Zanzibar.
Ajali ya MV Skagit ilitokea hivi karibuni katika Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar na kupoteza maisha ya Watanzania kadhaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment